Mahakama nchini Kenya imemzuia Rais William Ruto kuondoa marufuku ya takriban miaka sita ya ukataji miti.
Mahakama ya mazingira na ardhi iliamuru kuwa maamuzi ya rais kuwa watu waanze kukata miti tena izuiliwe kwa siku 14.
Kusitishwa kwa uvunaji miti ulipitishwa mwaka wa 2018 ili kuzuia kupunguka kwa misitu kwa haraka.
Alipokuwa akiondoa marufuku hiyo mwezi Julai, Ruto alisema ni "upumbavu" kuacha miti iliyokomaa kuoza huku viwanda vya mbao vikiagiza mbao kutoka nje na kwamba hatua hiyo itaongeza ajira nchini.
Chama cha Wanasheria nchini Kenya kilipinga uamuzi huo mahakamani, kikisema kuwa serikali haijatoa kesi ya kisayansi ya kuondoa marufuku hiyo au kushauriana na jamii vya kutosha kuhusu athari za kuanza kukata miti tena.
Katika uamuzi wake, wa Agosti 1, mahakama pia ilitoa maagizo ya kusitisha utoaji wa leseni za ukataji miti na serikali. Kesi hiyo itasikilizwa tena mahakamani Agosti 14.
"Tumewasilisha kesi nzuri na... amri ya muda ndiyo tuliyokuwa na matumaini kuwa mahakama itatupa," wakili wa jumuiya hiyo Kennedy Waweru aliambia AFP.
Misitu ya nchi
Wahifadhi walipinga vikali kuondolewa kwa marufuku hiyo wakisema ni kinyume na ahadi ya rais William Ruto ya kupanda miti bilioni 15 na kuimarisha misitu ya Kenya.
Lakini rais, ambaye ni mwenyeji wa mkutano wa marais wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi uliopangwa mwezi Septemba mjini Nairobi, alisema alisalia imara katika ahadi zake.
"Kumekuwa na wasiwasi juu ya uamuzi wetu wa kurejea kuvuta miti misituni " alisema Jumatano.
"Ili kuepusha mashaka, hatutageuza zoezi letu la upandaji miti. Tutahakikisha kwamba (kuondolewa kwa marufuku)... hakusababishi mathara mabovu kwa mazingira ambayo tumeona siku za nyuma ." rais aliongezea.
Miti ya kiasili
Mnamo mwaka wa 2018, serikali ilisema ukataji wa miti ya kiasili katika misitu ya Kenya ulikuwa "mkubwa" na kuonya kwamba hekta 5,000 kwa mwaka zilikuwa zikikatwa.
Katika wasilisho lake mahakamani, Chama cha Wanasheria nchini Kenya kilisema kuwa shughuli za ukataji miti "tayari zimeanza kwa dhati".
Ilisema marufuku hiyo iliondolewa kwa "kupuuza kabisa jukumu muhimu ambalo misitu inachukua katika kupunguza mabadiliko ya tabianchi, kuhifadhi bioanuwai, na kulinda mifumo muhimu ya ikolojia".
Sekta ya mbao nchini Kenya inaajiri watu 50,000 moja kwa moja na 300,000 kwa njia isiyo ya moja kwa moja, kulingana na takwimu za serikali.