Mahakama nchini Kenya imetupilia mbali fidia ya dola milioni 12 kwa waathiriwa wa sumu ya chuma ya lead katika mji wa pwani wa Mombasa.
Kemikali hiyo hatari, iliyoathiri takriban watu 3,000, ilitoka kwenye kiwanda cha kuchakata betri.
Siku ya Ijumaa, majaji wa mahakama ya rufaa waliamuru kesi isikilizwe upya katika mahakama ya mazingira kuhusu fidia inayolipwa kwa waathiriwa. Walisema kusikilizwa upya kunapaswa kuzingatia ushahidi wa ziada.
Wakaazi wa mtaa wa mabanda wa Uhuru Owino walishinda malipo hayo mnamo 2020 kufuatia mzozo wa kisheria wa miaka kumi ulioongozwa na mwanaharakati wa mazingira Phyllis Omido.
Katika kesi hiyo, walidai kuwa moshi na maji yanayotiririka kutoka kwa kiwanda hicho vimeathiri afya ya wakaazi wakiwemo watoto.
Mashirika ya serikali - yaliyokutwa na hatia ya kuzembea, pamoja na wakurugenzi wa kampuni - waliamriwa kulipa tuzo hiyo. Lakini walikata rufaa dhidi ya uamuzi huo uliopelekea uamuzi wa Ijumaa.