Mahakama ya Juu ya Kenya imeadhimisha miaka 12 tangu kuundwa kwake.
Katiba mpya ya Kenya ya mwaka 2010 iliruhusu kuundwa kwa Mahakama ya Juu ambayo inatambulika kama mahakama ya mwisho nchini humo.
"Wakati Mahakama inapopitia mamlaka yake ya kisheria, tunaialika ifanye upya nguvu zake katika kuunda mazingira yetu ya kikatiba. Ni lazima ibaki kuwa na kasi ya kufikiria mbele, yenye ubunifu na kuwajibika ili kukabiliana na changamoto za wakati wetu," Rais William Ruto alisema.
Majaji wakuu na washikadau wengine wa sheria wamefanya tathmini ya kazi za Mahakama ya Juu kupitia kongamano lake la kwanza kuwahi kutokea tangu kuanzishwa kwa Mahakama hiyo miaka 12 iliyopita.
Mada ya majadiliano imekuwa ni ‘Kutafakari na Kuchunguza Uamuzi wa Mahakama ya Juu ya Kenya: Miaka 12 ya Kutetea Katiba.'
"Safari ya Mahakama haijawa na changamoto. Tunapojitahidi kuimarisha sheria na kulinda Katiba, mahakama mara nyingi inaitwa kusawazisha maslahi na matarajio tofauti huku ikizingatia sheria. Ni muhimu kufahamu kwamba mamlaka ya Mahakama ya Juu kwa kiasi kikubwa ina mwelekeo wa kisiasa." Martha Koome, Jaji Mkuu katika Mahakama ya Juu amesema.
Mahakama ya juu imehusika katika kesi tatu za Uchaguzi Mkuu.
Mwaka 2013 iliamua kuwa Rais Uhuru Kenyatta alikuwa ameshinda Uchaguzi Mkuu kwa haki, dhidi ya Rail Odinga.
Mwaka 2017 Mahakama ya Juu ilibatilisha matokeo ya Uchaguzi Mkuu na kutaka uchaguzi mpya ufanywe. Hii ni baada ya mgombea urais Raila Odinga kupinga ushindi wa Uhuru Kenyatta. Mahakama hiyo iliamuru uchaguzi kurudiwa.
Katika Uchaguzi Mkuu wa 2022, Mahakama ya Juu nchini Kenya iliamua kuwa William Ruto alichaguliwa ipasavyo kuwa rais, na kutupilia mbali maombi kadhaa ya kutaka kubatilisha matokeo ya tarehe 9 Agosti 2022.
"Ikizingatiwa kwamba Mahakama hii hushughulikia masuala yanayohusu utawala, utumiaji wa mamlaka ya kisiasa, na malalamiko ya uchaguzi wa urais, Mahakama inaingia katika mizozo inayohusiana na utekelezaji wa mamlaka ya kisiasa. Hili bila shaka limepelekea Mahakama kudhalilishwa kisiasa na kuwa shabaha ya matamshi ya kisiasa katika mizunguko mitatu ya uchaguzi iliyopita," Jaji Koome aongezea.
Ameitetea Mahakama hiyo na majaji wake akidai kuwa hawashawishiki kamwe na siasa ila tu wanafuata matarajio ya kisheria.
"Ninataka kuchukua fursa hii kuwahakikishia Wakenya kwamba katika kutekeleza wajibu wetu, hatuvutiwi kufanya maamuzi ya kisiasa. Majaji hawaegemei upande wowote wa kisiasa na wanahusika na kuamua tu masuala ya kisheria na ushahidi mbele ya Mahakama bila kujali athari zao za kisiasa," Koome ameongezea.