Na Edward Qorro
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Ni mwaka mpya kwa Mahakama ya ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR), iliyo na makao makuu kwenye jiji la Kitalii na kidiplomasia la Arusha.
Hata hivyo, yawezekana kabisa hapakuwa na sababu yoyote ya kufurahi wakati chombo hicho cha kisheria kilicho chini ya mwamvuli wa Umoja wa Afrika, kilipofungua mwaka wake mpya siku chache zilizopita.
Ikumbukwe pia kuwa, AfCHPR ilikuwa inaadhimisha miaka 20, tangu kuanza kutumika kwa Itifaki ya Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu kuhusu Uanzishwaji ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, ambayo ilitiwa saini Januri 25, 2004.
Katika risala yake, Rais wa Mahakama hiyo Jaji Imani Aboud alioneshwa kusikitishwa na mwitikio hasi kutoka nchi wanachama za Umoja wa Afrika kuhusu uwepo wa taasisi hiyo ya haki.
“Tunauanza mwaka mpya tukiwa na changamoto zile zile tulizotoka nazo 2023, miaka 20 baadaye, ni nchi 34 tu kati ya 55 ndio zimeridhia itifaki hiyo,” alisema Jaji Aboud.
Kama hiyo haitoshi, kati ya mataifa hayo 34, ni nchi 8 tu ndio zimeridhia watu wake na mashirika binafsi kupeleka mashauri yao mbele ya Mahakama hiyo, kupitia kifungu 34(6) cha itifaki hiyo.
“Zaidi ya maamuzi 200 yamefikiwa na Mahakama hii tangu kuanzishwa kwake, hata hivyo, asilimia chini ya 10 ya maamuzi hayo ndiyo yametekelezwa na nchi wanachama,” alieleza Rais wa Mahakama hiyo.
Kwa mujibu wa Jaji Aboud, AfCHPR inashindwa kutekeleza majukumu yake kikamilifu kutokana na kukosekana kwa ushirikiano kutoka kwa baadhi ya wanachama wa Umoja wa Afrika.
Baadhi ya nchi zilizojitoa kwenye tamko la kuridhia watu binafsi na mashirika kupeleka mashauri yao yaliyokidhi vigezo katika Mahakama hiyo ni Rwanda iliyofanya hivyo mwaka 2016, ikifuatiwa na Tanzania ambayo ni mwenyeji wa AfCHPR mwaka 2019, Benin (2019) na Ivory Coast mwaka 2020.
Kulingana na wataalamu wa masuala ya Haki za Binadamu, maamuzi ya namna hii yanaiweka rehani dhana nzima ya ulinzi wa Haki za Binadamu na Watu barani Afrika.
Hakuna utashi wa kisiasa wala kipaumbele kwenye masuala ya Haki za Binadamu barani Afrika na hili linashuhudiwa na kutokuwa tayari kwa serikali za Afrika kuruhusu wananchi wake kuifikia mahakama hii
Ebby anasema kuwa kuna hofu kubwa kwa baadhi ya viongozi barani Afrika, ambazo nchi zao zinaongoza kwa ukiukwaji mkubwa wa Haki za Binadamu.
Hata hivyo, kuna kiwango kidogo sana cha uelewa wa kazi rasmi za Mahakama hii, kulingana na Ebby.
Tumekuwa tukisikia upotoshaji mkubwa kuwa baadhi ya nchi zilizoridhia itifaki ya kuruhusu watu kuifikia AfCHPR zinalenga kudhoofisha mahakama zao za kitaifa…hoja na hofu hizi hazina msingi hata kidogo kwani Mahakama ya Afrika inalenga kusaidia mahakama za kitaifa katika kuimarisha ulinzi wa Haki za Kibinadamu katika bara
Baadhi ya nchi, ikiwemo Tanzania, iliwahi kutetea maamuzi ya kujiondoa AfCHPR, ikidai kuwa inalinda uhuru wake.
Hata hivyo, kulingana na Ebby, sababu za namna hii ni mbinu tu ya baadhi ya nchi wanachama kukwepa kuwajibika kwa makossa ya ukiukwaji wa Haki za Kibinadamu.
“Inapaswa ieleweke wazi kuwa nchi zinapoidhinisha itifaki za Haki za Kibinadamu ndivyo zitakavyo legeza sehemu za mamlaka yao na kukubali kufungwa na kuwajibishwa na itifaki hizo,” anasisitiza Ebby.
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo wa mambo ya sheria, ni kanuni ya sheria ya kimataifa kwamba pindi nchi inapoidhinisha itifaki fulani, basi inalazimika kutii amri au maamuzi yanayotolewa na vyombo vilivyoanzishwa chini ya mkataba huo.
Kwa upande wake, afisa programu wa Chama cha Wanasheria wa Afrika Mashariki(EALS) Achilles Romwald nchi nyingi za Afrika ziliamua kuridhia itifaki hiyo kutokana tu na shinikizo kutoka nchi za magharibi, bila kusukumwa na utashi wa kisiasa.
Afisa huyo wa EALS anasema kuwa nchi nyingi za Kiafrika zimewekewa masharti ya kuheshimu na kulinda Haki za Binadamu ili waweze kupata misaada.
Suala la Haki za Binadamu halijapewa uzito wa kutosha hapa Afrika, tunajaribu kuficha ukweli kutokana na shinikizo la nchi za Magharibi
Romwald anasema nchi nyingi za Umoja wa Afrika hazitambui umuhimu wa haki, katika kuimarisha demokrasia na kuchochea ukuaji wa uchumi, kutokana na kukosekana kwa mbinu sahihi za utekelezaji na utoaji taarifa katika ngazi za kitaifa.
Mara nyingi, mchakato wa utekelezaji unahusisha idadi ya idara za serikali kuanzia wizara, sheria na idara za mahakama, na hakuna mifumo iliyoratibiwa miongoni mwa idara hizi katika ngazi ya kitaifa na hivyo kufanya shughuli ya utekelezaji wa maamuzi ya AfCHPR kuwa mgumu zaidi, anasema.