Mahakama Kuu nchini Kenya imeamuru kuachiliwa mara moja kwa watu sita, wanaodaiwa kutekwa nyara na mamlaka ya serikali.
Akitoa maagizo hayo, Jaji Bahati Mwamuyé pia alizuia kufunguliwa kwao mashtaka kusubiri matokeo ya kesi kuhusiana na hiyo iliyowasilishwa na Chama cha Wanasheria nchini (LSK).
Uamuzi huo wa mahakama umekuja baada ya cheti cha dharura kuwasilishwa na walalamishi hao ambao wamedai kuwa walizuiliwa kinyume cha sheria na polisi na vyombo vingine vya usalama.
Watu hao sita, ambao ni pamoja na Gideon Kibet na Bernard Kavuli. Wengine wanne - Peter Muteti, Billy Mwangi, Rony Kiplangat, na Steve Kavingo wanaripotiwa kuwa waathiriwa wa kutoweka kwa lazima na kuwekwa kizuizini kinyume cha sheria.
Jaji Bahati Mwamuyé ametoa amri ya Habeas Corpus inayotaka walalamishi wawasilishwe kortini kufikia saa 11:00 asubuhi Jumanne, Disemba 31, 2024, isipokuwa kama mamlaka itatoa sababu halali ya kuzuiliwa kwao.
Mahakama pia ilitoa amri ya kihafidhina ya kuwazuia polisi na walalamikiwa wengine kuwashtaki au kuwashtaki walalamikaji bila idhini ya Mahakama Kuu.
Maandamano Jumatatu
Wananchi waliandamana katika mji wa Nairobi kupinga utekaji nyara wa watu nchini. Polisi ililazimika kutumia nguvu kuwatawanya.
Takriban watu 10 walikamatwa katika maandamano hayo akiwemo wakili maarufu Okiya Omtata.
Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu ya Kenya imesema katika taarifa kuwa kumekuwepo na matukio kumi na tatu (13) zaidi ya utekaji nyara au kupotea kwa watu katika kipindi cha miezi mitatu na kufanya jumla ya kesi 82 kuanzia Juni 2024.
Kesi saba za utekaji nyara za hivi karibuni ziripotiwa katika mwezi wa Disemba 2024 ambapo sita kati yao wakiwa bado hawajulikani walipo, hivyo kufikisha idadi ya watu 29 ambao hawajapatikana tangu Juni 2024.