Mahakama Kuu ya Kenya, kanda ya Kerugoya imeliagiza Bunge la nchi hiyo kuandaa zoezi lingine la ushirikishwaji wa umma katika kila eneo bunge kuhusu kuondolewa madarakani kwa Naibu Rais, Rigathi Gachagua.
Agizo hilo linafuatia hati ya dharura iliyowasilishwa na mwakilishi wa wanawake katika eneo la Kirinyaga Jane Njeri Maina.
Kwa sasa, bunge la nchi hiyo limeandaa utoaji maono wa wazi wenye nia ya kuwapa wananchi fursa ya kutoa maoni yao kuhusu muswada wa kumuondoa naibu Rais Rigathi Gachagua madarakani.
Muswada huo, ambao tayari umewasilishwa bungen, unamtuhumu Rais Rigathi Gachagua kwa kukiuka sheria, kutoheshimu Katiba na Ofisi ya Rais na maafisa wengine wa serikali.
Bunge la nchi hiyo limeratibu ushiriki wa umma katika majimbo 290 ndani ya kaunti 47 nchini Kenya.
Jaji Richard Mwongo alisema mkutano wa hadhara uliopangwa kufanyika Oktoba 4, unaweza kuendelea kama hatua ya kwanza.
Ukumbi wa Bomas ulioko jijini Nairobi, ulifurika watu, waliokuwa tayari kutoa maoni yao.
" Ili tumalize ukabila Kenya na siasa ya kuchanganya watu, ni lazima Gachagua aachie ngazi," alisema Kasmuel MacOure, ambaye ni mkazi wa Nairobi.
“Kuna wabunge hawajawahi onekana bungeni, lakini leo wako mstari wa mbele kutoa maoni ya kumuondoa Gachagua madarakani,” alisema mkazi mwingine wa jiji hilo.
"Nilipiga kura moja, kama kundoka, basi waende wote," alisema mkaazi mwingine wa Nairobi.
"Naibu Rais Gachagua na Rais Ruto wote waondoke madarakani, kwa wabunge wetu mkirudi bungeni jua wananchi walisema nini. Mkishindwa kutuwakilisha tutarudi mitaani. Hatutovumilia ubadhirifu kwa kivuli cha uongozi," alisema mwananchi mmoja mkazi wa kaunti ya Machakos.
Wakenya walianza kumiminika mapema saa kumi na mbili asubuhi katika vituo tofauti nchini ili kujaza fomu zilizotolewa, huku zoezi la ushirikishwaji wa umma likipangwa kufanyika siku nzima.
Ushiriki wa Umma nchini kote unafaa kumpa kila mwananchi fursa ya kuchangia mchakato wa kuondolewa kwa Naibu Rais Gachagua. Haki hii ya kikatiba inahakikisha kwamba maamuzi yanaakisi matakwa ya wananchi.
"Serikali hii ilichaguliwa na sisi wenyewe. Ikiwa Gachagua ni mbaya, basi hata Ruto ni mbaya pia. Wote waende. Hakuna kubakisha mtu; afe dereva, afe na kondakta wake pia," alisema mwananchi mmoja aitwaye Peter Maina.
Ushiriki wa umma pia unatoa kwa Wakenya kutoa maoni yao kuhusu mienendo na sababu za kumbakisha Gachagua madarakani.
Na huko Mombasa, mkazi mwingine alikuwa na haya ya kusema:
"Wabunge wamewekeza nguvu kumtimua Naibu Rais Gachagua, lakini ombi langu ni kwamba wawekeze nguvu hizo katika masuala yanayowahusu Wakenya kama vile sakata la Adani na sekta ya afya. "
" Rais Ruto lazima aheshimiwe. Yeye ndio kiongozi wa nchi. Gachagua lazima amuombe Rais msamaha," aliongeza mkazi mwingine wa Mombasa.
"Jana usiku, watu walipiga kura kumuondoa Gachagua kwakuwa walipewa pesa. Lakini sisi kama wakaazi wa Laikipia, tunasema Riggy G lazima abaki," Wahome Marangi, mkazi wa Laikipia alisema.