Kesi ya ufisadi ya aliyekuwa Waziri wa Utalii Kenya Najib Balala imetupiliwa mbali na Mahakama / Picha: AFP

Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Malindi James Mwaniki, leo amemruhusu Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kuondoa Kesi inayoendelea dhidi ya aliyekuwa Waziri wa Utalii Kenya Najib Balala, aliyekuwa Katibu wake Mkuu na wengine 14.

Kesi ya ufisadi ya shilingi bilioni 8.5 ( zaidi ya $66 milioni) inawakabili aliyekuwa Katibu wa Baraza la Mawaziri, Wizara ya Utalii Bw. Najib Mohammed Balala na Katibu Mkuu wake Leah Adda Gwiyo.

Balala na washtakiwa wenzake walikamatwa na Tume ya Maadili na Kupambana na Rushwa, EACC, Disemba 22, 2023 na kushtakiwa kwa madai ya udanganyifu wa ununuzi na wizi wa pesa za umma katika ujenzi wa tawi la Pwani la Chuo cha Utalii cha Kenya (kilichopewa jina Ronald Ngala Utalii College) huko wilaya ya Kilifi.

EACC inasema ilipinga ombi la DPP la kuondoa kesi hiyo, ambayo ni kinyume na maslahi ya umma na kikwazo katika vita dhidi ya ufisadi.

Hakimu wa Kupambana na Ufisadi alikataa kukubali Hati ya Kiapo ya Mpelelezi wa EACC kupinga uondoaji huo.

Uchunguzi wa EACC ulithibitisha kuwa washtakiwa waliwezesha malipo yasiyo ya kawaida ya Ksh. Bilioni 8.5 ( zaidi ya $66 milioni) kupitia Wizara ya Utalii/ Picha kutoka Ronald Ngala Utalii College

Katika uamuzi wake, Hakimu Mashauri aliitaja sababu iliyotajwa na DPP kutaka kujitoa kwake ni ya kina na kwamba haikuonyeshwa vya kutosha kwa Mahakama kwa nini itakuwa vigumu kwa kesi hiyo kuendelea.

Mahakama, hata hivyo, iliwaachilia washtakiwa na iliamua kwamba uamuzi wowote wa siku zijazo wa kuwafungulia mashtaka upya juu ya ukweli huo itakuwa ni matumizi mabaya ya mchakato wa mahakama.

Mashtaka dhidi ya Balala na wenzake

Kulingana na EACC uchunguzi wa Tume uligundua kuwa Baraza la Mawaziri liliidhinisha ujenzi wa Chuo cha Utalii huko Vipingo kwa gharama ya Kes. bilioni 1.95 zaid ya $15.145milioni ) lakini gharama za mradi baadaye ziliongezwa na maafisa wa Wizara ya Utalii hadi shilingi bilioni 10.4 (zaidi ya $80,7 milioni) dhidi ya gharama iliyoidhinishwa.

Uchunguzi zaidi wa EACC ulithibitisha kuwa washtakiwa waliwezesha malipo yasiyo ya kawaida ya Kes. Bilioni 8.5 ( zaidi ya $66 milioni) kupitia Wizara ya Utalii, ambapo Kes.4 bilioni zililipwa kwa njia ya udanganyifu kwa kampuni ya Baseline Architects Limited kwa ajili ya huduma za ushauri katika ujenzi wa chuo.

Katika kikao cha Bodi ya uongozi wa bodi ya Chuo cha Ronald Ngala Utalii kilichohudhuriwa na Katibu wa Baraza la Mawaziri Najib Balala na Katibu Mkuu Leah Gwiyo, inadaiwa Bodi ilitupilia mbali miundo na mipango ya ujenzi iliyofanywa na Wizara ya Ujenzi na kuazimia kuwashirikisha washauri binafsi.

Hii ilkuwa kampuni ya Baseline Consortium iliyochaguliwa kuendeleza miundo mipya na kumsimamia mkandarasi mkuu, kwa gharama iliyozidishwa ya Kes.4 bilioni.

Mahakama ilitupilia mbali kesi hii siku ambayo kesi hiyo ilipangwa kutajwa ili kupanga tarehe ya kusikilizwa.

TRT Afrika