Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uratibu wa masuala ya kibinadamu inasema watu 45 wameuawa kutokana na mafuriko katika mkoa wa Somali nchini Ethiopia.
“Zaidi ya kaya 35,000 zimekimbia makazi yao, maisha ya watu 45 yamepotea, zaidi ya mifugo 23,000 iliangamia, na zaidi ya hekta 99,000 za mashamba kuharibiwa katika Mkoa wa Somali pekee,” inasema katika taarifa.
Mvua za kati ya Februari na Aprili zimewapa afueni maeneo yaliyokuwa na ukame hasa katika shughuli za kilimo, upatikanaji wa maji kwa wanadamu na mifugo, na malisho.
Hata hivyo mvua hii tena imeleta madhara kwa wengine.
Umoja wa Mataifa unasema mvua hii pia imesababisha hasara ya maisha , uharibifu wa makazi, shule, afya. Maelfu ya mashamba yenye mazao yalisombwa na maji. Mafuriko hayo pia yametatiza elimu ya watoto huku wakilazimika kutokwenda shule.
Mpango wa pamoja wa Serikali na mashirika ya kukabiliana na mafuriko uliotolewa mwezi Aprili unaomba dola za Marekani milioni 86 kusaidia zaidi ya watu 170,000 waliokimbia makazi yao.
Hata hivyo, tangu mwezi Aprili, takwimu hizi tayari zimepitwa na kiwango cha mahitaji yanayohusiana na mafuriko baada ya uharibifu zaidi kutoka kwa mafuriko katika ukanda wa Shabelle mkoani Somali nchini Ethiopia.