Kituo cha Utabiri wa Hali ya Hewa cha Kenya kimeonya kuwa mvua kubwa inatarajiwa kuendelea kunyesha katika maeneo mengi ya nchi.
"Mvua ya pekee zaidi ya milimita 20 huenda ikanyesha katika maeneo ya kati, Nairobi, Kaskazini-Mashariki, Bonde la Ufa, ukanda wa Pwani na nje ya pwani," imeonya katika taarifa yake mitandaoni.
Tahadhari hili inakuja huku mafuriko yakiendelea kuleta madhara katika sehemu tofauti ya nchi.
"Mvua kubwa na mafuriko yamesababisha zaidi ya watu 194,000 kukosa makazi na karibu 205,000 kuathiriwa nchini Kenya," Umoja wa Mataifa umesema.
"Wasaidizi wa kibinadamu wanaunga mkono serikali katika kuongeza juhudi za misaada. Msaada wa haraka wa chakula, maji, makazi, uokoaji na huduma za afya ni muhimu," imeoengezea.
Serikali inasema angalau wananchi wanazingatia onyo la kuhama kutoka maeneo ya mafuriko.
"Tunawapongeza Wakenya wenzetu kwa umakini wao wa ziada na kuitikia tahadhari ya mafuriko na maagizo ya kuhama," msemaji wa serikali ya Kenya Isaac Mwaura amesema katika mtandao wa X.
"Ushirikiano huu unazaa matunda kwani waathirika wa mafuriko wamepungua kwa kiasi kikubwa. Hata hivyo, tunaomboleza kifo cha mtu mmoja aliyefariki kwa kuzama katika kaunti ya Kirinyaga...Hii inaongeza idadi ya vifo vinavyohusiana na mafuriko hadi 229," Mwaura ameongezea.
Bado juhudi za kuokoa watu zinaendelea nchini kupitia Huduma ya Wanyamapori ya Kenya (KWS) ambayo imejitolea kuwaokoa watu waliokwama katika sehemu tofauti kwa sababu ya barabara kuzibwa na mafuriko.
"Jumapili timu yetu ilianza kazi huku Mto Nyando ukivunja kingo zake, na kuwaacha watu wengi kukwama katika eneo la Ahero Kaunti ya Kisumu. Tumetoa ndege zetu, tukistahamili anga yenye msukosuko ili kuwaokoa walio katika dhiki," KWS imesema.
"Eneo hilo bado halijatulia. Ujumbe wa Kijabe ulipokea mvua ya milimita 62.5 jana usiku na njia za chini za reli zinaendelea kujaa maji. Maporomoko ya matope ni suala la muda tu," Erik Hersman mtaalamu katika eneo la Kijabe lililoathiriwa anasema katika mtandao wake wa X.
"Zaidi ya hayo, kwa sababu ya misitu midogo iliyofunikwa kwenye ardhi ya juu, kiasi kikubwa cha maji na udongo kinaendelea kujaza mifereji ya maji," Hersman ameongezea.