Mafuriko yawaathiriki wengi Kenya na Somalia
Baadhi wamepoteza maisha huku maelfu wakikosa makazi kutokana na mvua zinazoendelea katika maeneo mbalimbali Afrika Mashariki.

"Mvua kubwa yenye athari tofauti za mafuriko zimeripotiwa kote nchini. Kufikia jana, kaya 15,264 zimeathiriwa, na majeruhi 15 wameripotiwa na angalau vifo 1067 vya mifugo. Ekari 241 za mashamba zimeharibiwa kutokana na mafuriko ya ghafla," limesema Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Kenya.

"Mji wa Diff ulioko Wajir Kusini umeathiriwa kabisa na mafuriko yanayosababishwa na mvua kubwa inayoendelea. Wakazi wengi wa mji huo wanaishi katika maeneo ya wazi," amesema mbunge wa eneo la Wajir Kusini Mohamed Adow.

"Ninatoa shukrani kwa Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya kwa hatua yake ya haraka katika timu za kuandaa kufanya tathmini ya hali hiyo na kwa kuhamasisha msaada unaohitajika sana. Diff inafikiwa tu kupitia helikopta kwa sasa na inaweza kuchukua muda kabla ya jamii kufikiwa na misaada," Adow aliongeza.

Mji wa Baidoa nchini Somalia

Mbali na Kenya, nchini Somalia, mvua kubwa ilinyesha katika Mji wa Baidoa, jimbo la Kusini Magharibi mwa Somalia, huku mafuriko yakiathiri makazi ya watu wasiokuwa na makao mnamo Novemba 5.

"Tangu Oktoba, zaidi ya watu 268, 200, hasa wakimbizi wa ndani, wameathiriwa na mvua kubwa inayosababishwa na El Nino na mafuriko ya ghafla katika jimbo hilo," Joyce Asha Francis Laku kutoka Shirika la UNOCHA amesema.

Wakati huo huo, nchini Tanzania kumeshuhudia mfululizo wa mvua katika maeneo kadhaa huku athari zikionekana katika jiji la kibiashara la Dar es Salaam pamoja na visiwani Zanzibar.

TRT Afrika