Mafuriko makubwa kutokana na hali ya hewa ya El Nino yamesababisha vifo vya watu 120 nchini Kenya, huku takriban watu 90,000 wakilazimika kuyahama makazi yao, serikali ilisema.
Idadi ya hivi punde inayokadiriwa ya vifo nchini Kenya imeongezeka maradufu kutokana na mvua kubwa za msimu kufuatia ukame mbaya zaidi kuwahi kutokea katika miongo minne.
Maelfu ya nyumba zimesombwa na maji , wakati mashamba yamezamishwa na makumi ya maelfu ya mifugo kufa maji, mashirika ya misaada yalisema.
Katika nchi jirani ya Somalia, mafuriko yamesababisha vifo vya takriban watu 96 na wengine 700,000 kuyahama makazi yao, afisa wa usimamizi wa majanga alisema.
Bwawa la Kiambere linaelekea kufurika
Kaunti nne mashariki mwa Kenya - Tana River, Garissa, Wajir na Mandera - ndizo zilizoathiriwa pakubwa, Waziri wa Mambo ya Ndani Raymond Omollo alisema.
"Mabwawa yote makubwa yanafuatiliwa, lakini Kiambere ina kiwango kidogo kilichosalia kufurika," Omollo alisema katika taarifa, akimaanisha bwawa la kuzalisha umeme katika mto Tana.
"Tunatoa wito kwa wale wanaoishi maeneo ya chini kuhamia maeneo ya juu hata kama serikali inaboresha uzalishaji wa umeme ili kupunguza changamoto."
Idara ya Hali ya Hewa ya Kenya ilitabiri kuwa mvua kubwa itaendelea kunyesha hadi Januari 2024.
Mabadiliko ya tabia nchi yanachangia madhara mengi mara kwa mara, kulingana na wanasayansi.
Viongozi wa Afrika wamependekeza kodi mpya za kimataifa na mabadiliko kwa taasisi za fedha za kimataifa ili kusaidia kufadhili mgogoro wa hali ya hewa.