Umoja wa Mataifa, imetangaza kuwa itatoa dola milioni 3 kwa ajili ya kuwasaidia waliaothiriwa.
"Mafuriko yanayosababishwa na El Nino yamezidi sana Kenya, nitatoa dola milioni 3 kutoka kopo la dharura la UN (UNCERF) kutoa msaada kwa watu 150,000 walioathirika," amesema Martin Griffiths, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa UN kwa Masuala ya Kibinadamu na Mratibu wa Misaada ya Dharura.
"Huku Kimbunga cha tropiki Hidaya kikitishia mvua kubwa zaidi, tunafuatilia kwa karibu hali hiyo na tuko tayari kujibu mara moja." Griffiths ameongezea.
Shirika la UN la watoto, UNICEF imepokea zaidi ya dola milioni 1 kutoka kwa ubalozi wa Uingerenza nchini Kenya. Ufadhili huo utawezesha usaidizi wa pesa taslimu kwa takribani kaya 6,900 katika kaunti zilizoathiriwa zaidi.
"Dharura zinapotokea, watoto ndio huathirika zaidi na wao ndio kipaumbele chetu cha kwanza," Shaheen Nilofer, mwakilishi wa UNICEF Kenya amesema katika taarifa.
UNICEF pia imesema itaongeza juhudi zake za kuzuia kipindupindu ili kuhakikisha afya na hali njema ya wale walioathiriwa inadumishwa na kusaidia kuzuia mlipuko wa magonjwa yatokanayo na maji.
Serikali nayo imetoa ahadi kwa waliaoathiriwa kuwa watatunzwa vizuri .
Rais William Ruto pia alieleza ya kuwa makazi mbadala yatatolewa kwa kaya 40,000.
“Aidha, tulitenga Sh1 bilioni kujenga upya shule ili watoto wetu waweze kuendelea na masomo yao kwa wakati unaofaa,” Rais Ruto alisema Jumatatu alipotembelea eneo la Kiamaiko na Mathare Depot katika Kaunti ya Nairobi wakati wa tathmini ya mafuriko katika eneo hilo
"Wale waliohamishwa kwa sababu ya usalama wao watakuwa na mahali pazuri pa kukaa. Kila familia itapata Sh10,000 (dola 74) kuwezesha jambo hili,” aliongeza Rais.
Huku rais akihakikishia kuwa kuna rasilimali ya kutosha kwa waathriwa wote, baadhi ya Wakenya hasa katika mitandao ya kijamii wameonyesha kutofurahishwa na uamuzi wake wa kuwapa wanaotafuta makazi mapya dola 74 tu, wengi wakidai ni kidogo sana.
Hali ya hewa kubadilika zaidi
Kufikia Mei 6, ripoti ya serikali inaonyesha ya kuwa karibia watu 223.198 walikuwa wameathiriwa na mafuriko katika sehemu tofauti ya nchini huku 229 wakipoteza maisha yao katika janga hilo.
Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa nchini Kenya, Kenya Met, imetahadharisha wananchi kuhusu ongezeko la baridi usiku katika baadhi ya maeneo ya nchi kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha.
Katika ushauri wake wa Jumatatu, Mei 6, Kenya Met ilibainisha kuwa halijoto katika baadhi ya maeneo haya inatarajiwa kushuka kutoka digri 8 mpaka10.
“Mvua inatarajiwa kuendelea kunyesha katika maeneo kadhaa ya nchi, vilevile mvua kubwa huenda kunyesha katika baadhi ya maeneo ya nyanda za juu za mashariki na magharibi mwa Bonde la Ufa, Bonde la Ziwa Victoria na Bonde la Ufa ," taarifa ya utabiri wa hali ya hewa imesema.
"Mvua kubwa inayotarajiwa kunyesha huenda ikaambatana na upepo mkali, ngurumo na radi. Wananchi wanashauriwa kuepuka kujificha chini ya miti na miundo ya chuma ili kupunguza uwezekano wa kupigwa na radi," sehemu ya ushauri ulisema.