Mto Tana, unaoenea hadi kilomita 1,000, ulifurika, na kuvunja kingo zake. Picha: Ali Wario. 

Wabunge wawili wa bunge kuu la Kenya na waakilishi wa wodi wawili na raia wengine ishirini na moja, walipotea baada ya safari yao ya kugawa chakula kwa waathiriwa wa mafuriko katika kaunti ya Tana River kabla ya mashua yao kutoweka.

Wabunge hao wawili, Ali Wario mbunge wa Garsen na Said Buya Hiribae wa Galole waliokolewa mapema Jumapili na kikosi kutoka shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya ambalo lilianzisha operesheni ya kuwaokoa.

Ali Wario mbunge wa Garsen akiwa na mwenzake Said Buya Hiribae wa Galole waliokolewa Jumapili. Picha: Hiribae (X)

Awali, mashua yao iliripotiwa kuishiwa na mafuta na kukwama majini, baada ya kupotea njia na kuwa ndani ya maji kwa saa nyingi Mto Tana.

Hali ya wasiwasi iligubika eneo la Tana River na taifa la Kenya baada ya taarifa za kutoweka kwa wabunge hao na wasaidizi wao ndani ya mto Tana kuenea.

Hata hivyo, mnamo usiku wa kuamkia Jumapili, waziri wa usalama wa ndani Kithure Kindiki, alitumia ukurasa wake kwenye mtandao wa (X) kuwahakikishia Wakenya kuwa abiria wa boti hilo walipatikana na walikuwa salama.

''Vyombo vya usalama vimefanikiwa kuwasiliana na abiria waliokuwa katika mashua ambayo ilipotea mapema jioni hii (Jumamosi) katika maji ya mto Tana,'' ilisema taarifa hiyo.

Jumla ya watu 21, wakiwemo wabunge hao wawili, maafisa mbalimbali na mtoto mdogo, waliokolewa na kikosi cha utafutaji na uokoaji la shirika la Msalaba Mwekundu, Kenya red cross

Kwa mujibu wa serikali ya Kenya, mafuriko hayo yanayoendelea kushuhudiwa Kenya, yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 140 kufikia Ijumaa, huku takriban watu nusu milioni wakilazimika kuhama makwao.

TRT Afrika na mashirika ya habari