Chama cha madaktari wa mifugo cha Kenya, yaani Kenya Veterinary Association, KVA kinaiomba serikali ya nchi hiyo kuahirisha zoezi la utoaji wa chanjo ya mifugo kwa wingi baada ya zoezi hilo kuzua utata.
"Serikali inapaswa kusimamisha utekelezaji wa sasa kwa muda wa kutoa chanjo hadi muda wa kutosha wa kuhamasisha umma na kushughulikia masuala kutoka kwa Wakenya," KVA imesema katika taarifa.
Serikali inakumbwa na shutuma tofauti hasa kutoka kwa wamiliki wa mifugo ambao wanapinga maagizo ya kulazimishwa kuwapa mifugo yao chanjo.
Serikali inakusudia kutoa chanjo kwa takriban ng'ombe milioni 22 na kondoo na mbuzi milioni 50 kuanzia Januari 2025 ikigharimia gharama yote.
"Ili kuhakikisha wakulima wananufaika kikamilifu na fursa za kimataifa, tutatekeleza mpango mpana wa chanjo, kwa kutumia chanjo zinazozalishwa nchini, ili kupunguza kuenea kwa magonjwa kulingana na viwango vya kimataifa," amesema Rais William Ruto akiwa katika kaunti ya Baringo.
Lakini Wakenya wa tabaka mbali mbali wamepinga chanjo hiyo wakidai kuwa chanjo hiyo imegubikwa na siri nyingi, huku wengne wakisema hawaelewi kwa nini serikali inawalazimisha.
Kwa upande wake, Chama cha Madaktari wa Mifugo cha Kenya, kinasema kwa kawaida chanjo ya wanyama hutolewa kwa lazima pindi panapokuwa na hatari katika eneo maalamu.
"Serikali inafaa kufuata njia ya msingi ya hatari ambayo inazingatia ugonjwa kuenea katika maeneo maalum badala ya chanjo ya jumla ya ugonjwa katika maeneo ambayo ugonjwa huo sio changamoto kubwa," taarifa yake imesema.
Rais amesema wanaopinga chanjo hiyo wanaendeleza porojo wakitaka umaskini uendelee Kenya.
" Sasa wewe, chanjo inafanywa hata ya binadamu hakuna mtu Kenya (ambae) hajapata chanjo. Kama si hatari kupea (kuwapa) wanadamu chanjo, itakuaje hatari kutoa chanjo kwa wanyama? " Rais Rutoa aliuliza katika hotuba yake.
"Na wanasema mambo ya ajabu, eti ng'ombe akipata hii chanjo atakosa kujamba, sasa mimi nauliza jameni, kwani sisi wote ambao tumepata chanjo kuna mtu amekosa kujamba kwa sababu alipata chanjo? Hii ni upuuzi aina gani?" alihoji Rais Ruto.
Serikali inasema imewahakikishia Wakenya kuwa chanjo zitakazotumika katika zoezi lijalo la chanjo ya mifugo nchini kote zimetolewa mashinani na Taasisi ya Kuzalisha Chanjo za Mifugo nchini (KEVEVAPI).
Katibu wa Baraza la Mawaziri la Kilimo na Maendeleo ya Mifugo Dkt. Andrew Karanja aliwatoa hofu kwamba chanjo hizo zitanunuliwa kutoka nje ya nchi, huku akieleza kuwa KEVAVAPI imekuwa ikizalisha na kusafirisha chanjo za mifugo katika nchi za Afrika kama Uganda na hata Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Amesema kutoa chanjo ya jumla ni kuwa na mtazamo mmoja kama nchi katika udhibiti wa magonjwa ya mifugo kama 'Foot and Mouth' kwa ng'ombe na 'Peste des Petits Ruminants (PPR)' kwa kondoo na mbuzi.
“Kilichokuwa kikifanyika siku za nyuma ni kwamba kaunti binafsi zimekuwa zikiwachanja mifugo yao wanapokumbwa na mlipuko wa magonjwa na kaunti inayofuata haitoi chanjo. Hili halijafanikiwa kwa vile mifugo mingi inasafirishwa kutoka kaunti moja hadi nyengine na hivyo basi inakuwa ni upotevu wa rasilimali ikiwa kaunti zote hazitachanja,” Waziri huyo alielezea.
Mkurugenzi Mtendaji wa KEVEVAPI Alex Sabuni alitoa hakikisho kwamba wana uwezo wa kuzalisha dozi milioni 22 zinazohitajika katika zoezi la chanjo nchi nzima.
Sabuni alieleza kuwa nchi imekuwa ikizalisha chanjo ya ugonjwa wa 'Foot and Mouth', inayotumika kwa ng’ombe, kondoo, mbuzi na nguruwe tangu mwaka 1964, katika kituo chao kilichoko katika eneo la viwanda Nairobi, huku kwenye kiwanda chao cha Kabete, mjini humo wanazalisha chanjo nyingine 12.