Madaktari na watalaamu wa afya nchini Kenya wameazimia kuendelea na mgomo wao ambao ulianza 13 Machi 2024, huku wakishinikiza kutimizwa kwa makubaliano yao na serikali ya mwaka 2017.
Hata hivyo, Serikali imeshikilia msimamo wake wa kutotimiza masharti hayo huku Polisi ikitoa onyo kuwa maandamano yao hayataruhusiwa.
" Wataalamu wa matibabu wanaendelela kufanya maandamano bila kuwataarifu polisi," taarifa kutoka huduma ya taifa ya polisi imesema.
" Tunawaomba madaktari wote wajiepushe na kukiuka haki za wengine wakati wa kuandamana na kwamba juhudi zao za kuvuruga uendeshaji mzuri wa hospitali hazitavumiliwa," taarifa hiyo imesema.
Lakini uongozi wa Muungano wa Madaktari, Wafamasia na Madaktari wa Meno nchini Kenya, KPMDU unasema hawatotetereka katika maamuzi yao.
" Si vitisho wala uonevu wowote utakaotufanya tusitishe mgomo huu," Davji Atellah mkurugenzi mkuu wa KPMDU amewaambia waandishi wa habari.
" Tutalazimika kuketi na kuwa na makubaliano ya kurudi kazini ambayo kwa hakika yanaelezea ulinzi wa makubaliano yetu na serikali ya 2017, ambao ulitiwa saini. Ili mgomo huu umalizike, inabidi kuwe na kipaumbele kwa wahudumu wa afya," ameongeza.
Huduma katika hospitali za umma na vituo vya afya vimeathiriwa huku wagonjwa wakikosa huduma mbalimbali.
Rais William Ruto aliwaambia madakitari wakubali kuishi kwa kiwango kilichopo cha malipo. Hata hivyo, watoa huduma hao wa afya, wanadai kuwa serikali imekiuka makubaliano ya mwaka 2017.
Mataalam hao wa afya wanaitaka serikali kuwatuma kazini wanafunzi wahudumu wa afya mara moja na kufuta malimbikizo ya mishahara ya madaktari kulingana na Makubaliano ya Pamoja ya 2017.
Wahudumu wa afya ambao wamehudumu kwa miaka minne chini ya kandarasi katika taasisi za afya ya umma wanadai ajira ya kudumu ambayo walikuwa wamehakikishiwa na serikali ya Kenya kufuatia miaka mitatu ya huduma.
Masuala muhimu yaliyoibuliwa na KMPDU ni pamoja na kucheleweshwa kwa kazi ya kuajiriwa hasa kwa madaktari wapya waliomaliza masomo yao.