Wafuasi wa upinzani wamekuwa wakifanya maandamano ya vurugu mitaani tangu kutolewa kwa matokeo ya uchaguzi mwezi Oktoba. /Picha : Reuters

Rais wa Zimbabwe na mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), Emmerson Mnangagwa, ameelezea utayari wa kambi hiyo kuunga mkono serikali inayokuja na watu wa Msumbiji katika kuimarisha demokrasia yao ya uchaguzi.

Katika taarifa iliyotolewa siku ya Alhamisi kwenye mtandao wa X, Rais Mnangagwa alikubali uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu siku ya Jumatatu, ambalo lilimthibitisha Daniel Chapo wa chama tawala cha Mozambique Liberation Front (Frelimo) kama mshindi wa uchaguzi wa urais wa Oktoba 9.

Msumbiji imekumbwa na maandamano makubwa tangu mwishoni mwa Oktoba, wakati mamlaka ya uchaguzi ilipomtangaza Chapo mwenye umri wa miaka 47 kuwa mshindi kwa kupata asilimia 71 ya kura, na kumshinda mgombea wa upinzani Venancio Mondlane wa Chama cha Optimist for Development of Mozambique (Podemos) ambaye alipata 20%.

Maandamano mapya

Mondlane alikataa matokeo, akishutumu wizi mkubwa wa kura na kuwataka wafuasi wake kuandamana. Mahakama kuu ilipewa jukumu la kusimamia kesi hiyo.

Maandamano mapya yalizuka Jumatatu baada ya uamuzi wa mahakama hiyo, ambayo ilithibitisha ushindi wa Chapo lakini ukarekebisha asilimia yake ya ushindi kutoka 71% hadi 65%.

Kulingana na Plataforma DECIDE, kikundi cha waangalizi wa uchaguzi, takriban watu 248 wamepoteza maisha katika siku 65 tangu maandamano yaanze.

Siku ya Jumatano, watu 33 waliuawa wakati mamia ya wafungwa walipotoka katika Gereza Kuu la Maputo huko Matola, lililoko takriban kilomita 15 (maili 9.3) kutoka mji mkuu.

Mkuu wa polisi Bernardino Rafael alithibitisha kuwa wafungwa 1,534 walitoroka, wakiwemo magaidi 29 "hatari sana", jambo lililozua wasiwasi mkubwa wa usalama.

Kutii uamuzi wa mahakama

Mnangagwa alisisitiza kuwa uamuzi wa mahakama kuu unakamilisha mchakato halali wa kuamua matokeo ya uchaguzi kwa kuzingatia sheria za kitaifa za Msumbiji na miongozo ya uchaguzi ya SADC.

“Kwa hiyo SADC inatarajia pande zote katika mchakato wa uchaguzi, kibinafsi na kwa pamoja, kutii uamuzi wa mahakam, ambao unapaswa kutoa njia ya kikatiba ya nchi na kuwezesha njia ya amani zaidi, na utulivu kwa maslahi ya wananchi wote wa Msumbiji,” alisema.

Rais pia aliitaka jumuiya ya kimataifa kuheshimu mamlaka ya Msumbiji na matakwa ya watu wake, akitoa wito kwa pande zote kuunga mkono amani, sheria na utulivu, ambayo nchi hiyo inahitaji haraka.

"Eneo letu limeshuhudia idadi kubwa ya chaguzi za kitaifa katika miaka miwili iliyopita, ushahidi wa kuimarika kwa mizizi na kustawi kwa demokrasia katika kanda yetu ya SADC," Mnangagwa aliongeza.

Maelfu wanaikimbia Msumbiji

Wakati huo huo, maelfu ya raia wa Msumbiji wamekimbia ghasia zinazoendelea hadi nchi jirani ya Malawi, maafisa wa serikali waliiambia Anadolu siku ya Alhamisi.

Dominic Mwandira, ofisa mwandamizi katika wilaya ya Nsanje nchini Malawi, ambayo inapakana na Msumbiji, alithibitisha kuwa karibu kaya 2,000 zimevuka na kuingia Malawi tangu Jumatatu.

"Wanakuja kama familia, na hadi sasa, tumewahifadhi shuleni tukingoja mipango ifaayo. Idadi hiyo huenda ikaongezeka,” Mwandira alisema katika mahojiano ya simu na Anadolu.

TRT Afrika