Zaidi ya wajumbe 30 000 wanahudhuria mkutano wa siku tatu jijini Nairobi kujadili mabadiliko ya Tabia nchi / Picha : X - Ikulu Kenya

Mkutano wa kwanza wa ngazi ya juu wa hali ya hewa barani Afrika umeanza Jumatatu katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, huku wajumbe wakilenga kuweka msimamo mmoja kabla ya mikutano ijayo ya kimataifa na kujadili jinsi ya kufadhili vipaumbele vya mazingira katika bara hilo.

Mwenyeji wa mkutano huo, Rais William Ruto, ambaye pia ndiye mwenyekiti wa kamati ya viongozi wa Afrika juu ya mabadiliko ya tabia nchi, amesema kuwa wakati umefika kwa Afrika kuhusishwa kikamilifu na kusikilizwa kama mmoja wa wadau wenye suluhisho.

''Mgogoro wa tabia nchi haubagui kati ya mataifa tajiri na mataifa maskini,'' alisema Rais Ruto.

"Hatua madhubuti ya hali ya hewa lazima itambue tishio letu la pamoja na pia fursa ya pamoja ya kukuza na kutekeleza suluhisho za pamoja za kimataifa.'' Aliongeza.

Rais William Ruto ametoa wito kwa wadau wa mazingira kuitambua Afrika kam abara lenye suluhishio badala muathiriwa tu wa ukame na njaa / Picha X- William Ruto 

Zaidi ya marais 20 na wakuu wa serikali wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo ambapo wanatarajiwa kutoa tamko la pamoja kuelezea msimamo wa Afrika kabla ya mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi, mjini New York nchini Marekani.

Akihutubia kikao wakati wa ufunguzi wa mkutano, waziri wa mazingira wa Kenya, Soipan Tuya amesisitiza kuharakishwa kwa upatikanaji wa suluhisho kwani unatishia usalama wa watu.

''Mjadala wa mabadiliko ya hali ya hewa umeingia katika enzi mpya. Sio tu kushughulikia tatizo la mazingira au maendeleo, lakini kuhusu kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa katika muktadha wa haki," Tuya alisema.

Rais William Ruto wamewataka vijana kuhusishwa katika mstari wa mbele katika kutafutia bara Afrika Suluhisho / Picha: X- William Ruto 

Wakati huo huo Rais WIlliam Ruto ametoa wito kwa vijana barani Afrika kujiweka mstari wa mbele katika kuokoa bara ili kuepukana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

''Vijana - kwa nguvu zao, bidii na werevu - lazima wachukue mamlaka na wajiweke katikati ya kuendesha simulizi hii mpya kuhusu bara letu,'' alisema Rais Ruto.

Rais Ruto aliongeza kuwa, ''Vijana wa umri huu wana nguvu kubwa kiasi kwamba sauti zao haziwezi tena kuachwa pembezoni.''

Kauli hii imeendana na wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliyesema kuwa vijana wakipewa fursa ya kuchangia, na kuwezeshwa kwa uwekezaji, suluhisho itapatikana kwa haraka.

Rais Ruto amewasili mkutanoni na Gari ya umeme Picha: Ikulu

Bwana Guterres ni miongoni mwa wageni mashuhuri watakaohudhuria kongamano hilo jijini Nairobi

TRT Afrika