Wachuuzi wa mboga jijini nairobi wanatatizika kuendeleza biashara zao kutokana na gharama kubwa/Picha TRT Afrika    

NA DAYO YUSSUF

Asubuhi na mapema kabla jua halijachomoza, Nuria anaungana na wachuuzi wengi hadi 'Marikiti' soko kuu jijini lililopewa jina la kutohoa kutoka Kiingereza kumaanisha Market yani soko, ambapo hununua mboga kwa wingi ili kuja kuuza rejareja kwa wateja wake karibu na nyumbani kwake.

Amekuwa akifanya hivi kwa miaka 7 iliyopita, na kwa uchungu ameona biashara ikizidi kuwa mbaya zaidi.

''Nimewalea watoto wangu kwa pesa ninazopata kutokana na biashara hii. Ilikuwa inatosha,'' anaiambia TRT Africa. ''Lakini sasa ninahofia huenda nitalazimika kutafuta kitu kingine cha kufanya. Kila kitu ni ghali.''

Mara nyingi ameenda sokoni na kurudi mikono mitupu. Labda bei zilikuwa juu sana au hakuweza kupata mboga anazouza.

''Nilikuwa nikinunua gunia dogo la vitunguu kwa shilingi 1200 ($9) lakini sasa nanunua kwa shilingi 2800 ($19).'' Anasema. ''Nikinunua kwa bei hiyo, nitauza kiasi gani kwa wateja wangu?''

Athari za ukame zinaonekana kwa wakazi wa eneo hilo kwani chakula ni adimu na bei haivumiliki / Picha : TRT Afrika

Tatizo limeenea katika maeneo mengi ya nchi na hata kuvuka mipaka. Wakulima wanasema, hawavuni sana kama walivyokuwa wakifanya. Wakati mwingine, mazao yote hushindwa kwa msimu.

'Mabadiliko ya hali ya hewa yanajadiliwa katika ngazi za juu na viongozi wa serikali, mashirika ya kimataifa au wanaharakati. Si kwa sababu wanashughulikia matatizo yao wenyewe, lakini kimsingi hili ni jambo ambalo linaathiri moja kwa moja mtu wa kawaida, au mtumiaji kijijini,'' anasema Ellen Otaru, mtaalamu wa mazingira nchini Tanzania.

''Kila mtu ameathirika kuanzia mkulima, mvuvi, mfugaji nyuki na mwingine yeyote anayetegemea maliasili kuishi.'' Otaru anaiambia TRT Afrika.

Kwa upande mmoja, mvua imefeli, mashamba yamekauka na hakuna cha kuvuna. Wakati huo huo upande wa pili, maji ya mafuriko yanasomba mimea na kuwalazimisha watu kukimbia kuokoa maisha yao. Ikiwa Mabadiliko ya Tabianchi yangekuwa na uso, hii ndio uso wake halisi.

Uzalishaji  wa viwanda vikubwa na gesi chafuzi zina athari mbaya kwa mazingira./ Picha Reuters

Nguvu zote zinahitajika wakati jamii ya kimataifa inapoungana kupigana na janga hili. Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuhusu mstakabali hatari na kutaka suala hili lipewe kipaumbele cha juu zaidi duniani.

Kwa vyovyote vile, Nuria haelewi bado ni kwa nini hawezi kununua mboga kama zamani. Anaendelea kulalamikia 'wakulima walafi' ambao wanapandisha bei.

Wiki iliyopita, kumekuwa na zogo jijini Nairobi kuhusu ujio wa viongozi wa dunia kujadili Mabadiliko ya Tabianchi na suluhisho zinazowezekana. Nuria anasema ameiona kwenye habari za jioni, lakini haoni yanamhusu vipi.

''Tunachofanya kwa namna yetu ndogo hatimaye huchangia katika matatizo ya kimataifa,'' anasema mtaalam Ellen Otaru. ''Maji hayazalishwi katika viwanda, hivyo unapopoteza maji nyumbani, yanapunguza hifadhi kuu. Sasa kama hakuna mvua tunaijazaje hiyo tena? Ukiwasha taa bila sababu siku nzima, inachangia ongezeko la joto.'' aeleza Bi Otaru.

''Uzalishaji wa viwanda vikubwa na gesi chafu vina athari mbaya kwa mazingira. Lakini sote tunachangia kwa njia zetu wenyewe kwa uchafuzi wa mazingira. Labda pia tuchangie kwa njia zetu wenyewe kuokoa dunia,'' anaongeza Otaru.

Athari inayotiririka

Masuala makuu ya kimataifa kama vile mabadiliko ya hali ya hewa, ongezeko la joto duniani, na nishati ya kijani, hayahitaji kujadiliwa kwa faragha. Wataalamu wanasema kadiri inavyojumuisha zaidi, ndivyo masuluhisho yanavyoweza kupatikana kwa haraka.

Wataalamu wanatoa wito kwa ushirikishwaji katika kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa kwa masuluhisho ya dharura zaidi / Picha : AP

''Kama mtu wa kawaida katika kijiji na sielewi mabadiliko ya hali ya hewa, na jinsi yatakavyoathiri maisha yangu, sitaweza kurekebisha maisha yangu ipasavyo,'' anasema Otaru. ''Ni vyema kwamba mazungumzo mengi sasa yanatoa wito kwa wanawake kushiriki.''

Kutoka kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Marais wa Kenya na Tanzania au hata Mke wa Rais wa Uturuki, Emine Erdogan, kuna wito wa dharura kwa wanawake kujitokeza na kuchukua jukumu la kupambana na mzozo huo.

Wanawake wanasemekana kubeba mzigo mkubwa zaidi wa Mabadiliko ya Tabia Nchi.

''Mwanamke anapoelewa Mabadiliko ya Tabianchi, itamsaidia kuepuka migogoro nyumbani kwake, na unyanyasaji wowote wa kijinsia'' anasema Otaru. ''Kama familia haiwezi kuendeleza maisha yao hasa katika familia zinazotegemea kilimo, kama hakuna pesa, hakutakuwa na amani katika familia hiyo.''

Otaru anahusisha baadhi ya matatizo ya familia kama vile msongo wa mawazo moja kwa moja na ukosefu wa rasilimali au mapato duni. Na hili anasema linaweza pia kuwaathiri watoto katika familia.

''Wakati mwingine familia hulazimika kutengana kutokana na shinikizo za kiuchumi. Baba, ambaye alikuwa akifanya kazi katika shamba lake na familia yake anaamua kuhamia mjini kutafuta mapato mbadala, hii inaathiri watoto.’’ anaeleza.

Haba na haba hujaza kibaba

Utafutaji wa suluhisho sio lazima uwe katika kiwango cha mabilioni mengi. Kila mtu anaweza kufanya sehemu yake ndogo. Wataalamu wanasema, ni wakati wa kujumuisha akili za vijana pia.

Ni wakati wa kujumuisha akili za vijana katika mazungumzo ya mabadiliko ya hali ya hewa ili kujenga ufahamu na kuwatayarisha kwa athari zisizoweza kuepukika kwa wataalam wa siku zijazo wanasema / Picha : Reuters

''Hili ni tatizo kwa wote. Ni muhimu kwa kila mtu kulielewa na kuhusishwa mapema katika umri wa shule ya chekechea na kumfanya aelewe kwamba ana jukumu la kutekeleza katika kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa,'' anasema Ellen Otaru. ''Lakini muhimu zaidi anahitaji kujifunza kuzoea kuishi kulingana na maendeleo yanayomzunguka kurekebisha maisha yake kulingana na mabadiliko ya tabia nchi,'' anaiambia TRT Afrika.

Benki ya Dunia inaeleza kuwa Afrika itakuwa na zaidi ya asilimia 40 ya vijana katika nchi za kipato cha chini na cha kati ifikapo mwaka 2050. ''Mikakati madhubuti inahitajika ili kuhakikisha mahitaji ya kimsingi ikiwa ni pamoja na chakula, kwa mantiki hiyo ipo haja ya kujipanga kuhakikisha mifumo ya chakula inaendelea kuwa shwari'' inaendelea kusema.

Mwisho wa siku, Nuria mjini Nairobi anafunga mboga zake kwenda nyumbani. Hakuuza sana lakini hashangai.

''Siku hizi watu hata hawanunui bidhaa kama nyanya. Nitaacha kuwaletea,'' anasema. '' Baada ya yote ni ghali sana.''

Huku siku ya pili ya mkutano huo ikifungwa jijini Nairobi, wajumbe wanarejea. Vyombo vya habari vimezagaa taarifa za mipango ya utekelezaji kwa siku zijazo.

Nuria anafuatilia taarifa hizi pamoja na familia yake ili kujifahamisha kile kinachoendelea, lakini itachukua muda zaidi na juhudi nyingi zaidi kumfanya ashiriki katika kampeni ya kuokoa ulimwengu.

TRT Afrika