Mgomo huo ulioanza Machi 14, umekuwa na athari kubwa kwa mfumo wa huduma za afya/ Picha : Reuters 

Muungano wa Maafisa wa Kliniki nchini Kenya (KUCO) umetangaza kujiunga katika mgomo wa madaktari unaoendelea kuanzia Jumatatu.

Maafisa hao wa Kliniki wanasema mgomo huo umechochewa na kile wanachodai kuwa kuzembea kwa serikali katika sekta ya afya.

Muungano huo pia umebainisha kuwa maafisa wa kliniki kitaifa watagoma wote isipokuwa wale wanaofanya kazi katika hospitali kuu za rufaa, Kenyatta jijini nairobi na Moi, jijini Eldoret.

Katibu Mkuu wa KUCO George Gibore na Mwenyekiti Peterson Wachira wamelalamika pia kuwa juhudi zao zimekuwa zikitatizwa na magavana wa majimbo ambao wamechelewesha zaidi mazungumzo ya nyongeza y amishahara miongoni mwa mengine.

KUCO pia inataka kuajiriwa mara moja kwa maafisa wa kliniki 20,000, kuambatana na Wizara ya Afya kwa miongozo iliyoidhinishwa ya uanzishaji wa wafanyikazi wa mafunzo ya 2020 pamoja na kuidhinishwa kwa Miongozo ya Kuendeleza Kazi kwa maafisa wa kliniki.

Uamuzi wa kusitisha huduma za dharura unakuja huku madaktari wakiitaka serikali kushughulikia malalamishi, hasa kuhusu kucheleweshwa kwa ajira ya wanafunzi waliohitimu udaktari.

Kuchelewa huko kunadaiwa kusababisha upungufu wa wafanyikazi na kucheleweshwa kutumwa kwa wahudumu wa matibabu 1,200 katika hospitali.

Mgomo huo ulioanza Machi 14, umekuwa na athari kubwa kwa mfumo wa huduma za afya, huku hospitali zikilazimika kuwafukuza wagonjwa au kufanya kazi na wafanyikazi na rasilimali chache.

Licha ya hayo, kumekuwa na vuta nikuvute kati ya waziri wa afya Susan Nakhumicha na wawakilishi wa muungano mbali mbali za wahudumu wa afya, ambapo wakayi mwingine mikutano imekatishwa ghafla kwa kujiondoa waziri kutokana na kutoelewana.

TRT Afrika