Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amemteua balozi Taye Atske Selassie kuwa Waziri wa Mambo ya Nje.
Bunge la taifa wakati wa kikao chake cha kawaida asubuhi ya leo, liliidhinisha uteuzi wa Balozi Taye Atske Selassie kuwa Waziri wa Mambo ya Nje.
Hapo awali, Balozi Taye alishika wadhifa wa Mwakilishi wa Ethiopia katika Umoja wa Mataifa.
Atsake anachukua nafasi ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ye Nje Demeke Mekonnen aliyejiuzulu kutoka nafasi yake mwezi Januari mwaka huu.
Mekonnen pia aliwahi kuwa naibu waziri mkuu wa nchi. Nafasi hii sasa imechukuliwa na Temesgen Tiruneh, mkurugenzi mkuu wa zamani wa Huduma za Kitaifa za Ujasusi na Usalama (NISS) kama naibu Waziri Mkuu.
Wataalamu wa siasa wanasema kujiuzulu kwa Mekonnen kutoka kwa nyadhifa zake huenda ikawa kwa sabaabu ya vita vinavyoendelea kati ya jeshi la serikali na wapiganaji kutoka eneo la Amhara.
Mekonnen ni wa kutoka eneo la Amhara na amekuwa akipokea shutuma kutoka kwa watu wa eneo hilo wakidai kuwa anaunga mkono serikali ambayo inawakandamiza.
Mabadiliko mengine makuu yametokea katika wizara ya afya, ambapo bunge imeteuwa waziri mpya.
Bunge limeidhinisha uteuzi wa Dk. Mekdes Daba ambaye sasa anachukua nafasi ya Waziri wa Afya Lia Tadesse.
Taddesse alikuwa waziri wa afya tangu mwaka 2020 wakati ambapo Ethiopia ilikuwa inakumbana na Uviko 19 na pia vita vikali kati ya jeshi la serikali na kikundi cha Tigray kaskazini mwa nchi.
Waziri huyu mpya wa afya alikuwa na nafasi ya juu katika Ofisi ya Naibu Mkurugenzi Mkuu katika makao makuu ya Shirika la Afya Duniani (WHO) huko Geneva.