Jiji la Arusha limeweka historia ya aina yake siku ya Oktoba kwa kuleta pamoja zaidi ya magari ya 1,000 aina ya Land Rover kutoka sehemu tofauti, ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha tamasha la siku tatu, lilipewa jina la 'Land Rover Festival 2024'.
Kinachosubiriwa kwa sasa, ni kufahamu iwapo jiji hilo na kimsingi nchi ya Tanzania imefanikiwa kuvunja rekodi iliyokuwa inashikiliwa na jiji la Bavaria la nchini Ujerumani ambalo lilishuhudia mkusanyiko wa magari aina ya Land Rover yapatayo 632 mwaka 2018.
Jumla ya magari 1,000 aina ya Land Rover yanatarajiwa kukusanyika pamoja jijini Arusha, Tanzania siku ya Oktoba 12 hadi 14 katika tamasha lililopewa jina la ‘Land Rover Festival2024’, na hivyo kuweka rekodi mpya ya Guinness.
Watu mbalimbali, hususani wapenzi wa magari ya familia ya Land Rover, kutoka sehemu mbalimbali Afrika Mashariki na ulimwengu walishiriki tamasha hilo lililofanyika katika mji wa kitalii wa Arusha nchini Tanzania.
Mara baada ya kuingia kwa msafara maalumu, magari hayo yalielekea moja kwa moja kwenye viwanja wa Magereza vilivyopo katika eneo la Kisongo, jijini Arusha.
Siku ya Oktoba 13, msafara wa magari hayo utaelekea katika hifadhi ya Taifa ya Arusha, kwa ajili ya kufanya shughuli za kitalii.
"Tuna ndoto kama Taifa ya kuvunja rekodi ya Guiness iliyoandikwa na Ujerumani kwa kuwa na magari 632, sisi mkoa wa Arusha tunataka kuwa na magari 1000," alinukuliwa akisema Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Arusha siku ya Septemba 23, 2024.
Kulingana na Makonda, msafara wa huo wa Land Rover utakuwa na urefu wa kilomita zaidi ya 12 huku wakishiriki wakipata fursa pia ya kutalii bure kwenye hifadhi ya Taifa ya Arusha kwa kutumia magari yao huku pia kukitengwa maeneo mbalimbali ya kuburudika pamoja na maeneo kwaajili ya michezo ya watoto.