Rais Samia ameongoza viongozi wengine, wakiwemo wa sasa na waliostaafu katika maadhimisho ya miaka 60 ya JKT katika Uwanja wa Jamhuri Dodoma.
Rais Samia ameelezea matamanio yake kuona jeshi la Kujenga Taifa likiiimarika na kuwa la kisasa katika utendakazi wake.
''Mafunzo ya JKT ni sehemu muhimu ya mchango wa amani tulionao Tanzania.'' Amesema waziri wa Ulinzi wa Tanzania, Innocent Lugha Bashungwa, wakati wa maadhimisho hayo ya miaka 60 ya JKT, jijini Dodoma.
''Vijana wanaopita JKT wanapaswa kubeba dhima ya uzalendo mioyoni mwao siyo katika midomo kwani jeshi linawafanya vijana kuwa wamoja na wenye kuithamini nchi yao katika kuonyesha uzalendo.'' amesema Mama Samia, alipokuwa akihutubia hafla hiyo.
Waziri wa Ulinzi Innocent Bashugwa aliongeza kuwa, wizara yake itaendelea kushirikiana na wizara nyingine za kisekta kuboresha mafunzo stadi za kazi kwa vijana wa Jeshi la Kujenga Taifa na kuwawezesha kuwapatia ujuzi na maarifa zaidi ya ilivyo sasa ili baada ya kuhitimu mafunzo ya JKT waweze kujitegemea.
“Katika miradi mikubwa mmefanya vizuri sana ikiwemo ujenzi wa Ikulu ya Chamwino, sisi Serikali tutaendelea kuwaunga mkono na ikibidi mpate mikopo ili kuongeza nguvu ya uzalishaji tuko tayari kuwadhamini,” amesema Rais Samia.