Na Dayo Yussuf
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
''Mara tu dari ya glasi inapovunjwa, haiwezi kamwe kuunganishwa hata kama utajaribu vipi,'' Elen Johnson Sirleaf alikuwa akitoa hotuba ya TED miaka 4 iliyopita, maneno yake yakipasua hadhira ya waliokuwa wakimsikiliza kwa hamu hasa wanawake na wasichana.
Kwa wanawake wengi, Elen Johnson si mzungumzaji tu, lakini dhihirisho la kweli la ‘kile ambacho wanaume wanaweza kufanya, wanawake wanaweza kukifanya vyema zaidi.’’
Aliyekuwa Mshindi wa Tuzo ya Nobel na rais wa kwanza Mwanamke barani Afrika amekuwa mstari wa mbele katika uongozi, akiendesha mageuzi, mabadiliko na kuvunja vikwazo.
Lakini Afrika inapopambana na changamoto za kijamii, kisiasa na kiuchumi, suala la wanawake kuingia katika uongozi halijawahi kuwa muhimu zaidi.
Kihistoria, uongozi katika bara hili umetawaliwa na wanaume, lakini idadi inayoongezeka ya wanawake wanasonga mbele, ikionyesha kwamba sio tu wanahusika katika majukumu ya uongozi lakini mara nyingi wana nafasi ya kipekee kuleta mabadiliko ya maana.
"Nilikuwa rais wa kwanza mwanamke wa taifa la Kiafrika, na ninaamini kuwa nchi nyingi zinafaa kujaribu hilo," Bi. Sirleaf anatupa changamoto kwa wasikilizaji wake katika mazungumzo ya TED na Afrika nzima.
Sio mmoja sio wawili
Na kuna wanawake wengi zaidi ambao wamepiga hatua na kufanikiwa kuendesha njia yao katika eneo lililotawaliwa zaidi na wanaume.
Rais Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa kama Rais wa Tanzania akikanyaga viatu vya mtangulizi wake John Pombe Magufuli aliyefariki dunia akiwa madarakani. Na sio mbali sana, Kusini, Netumbo Nandi-Ndaitwah: hivi karibuni alichaguliwa kuwa Rais wa kwanza mwanamke wa Namibia, na kupata asilimia 57 ya kura.
Rwanda, ambayo mara nyingi inasifiwa kwa sera zake za kimaendeleo, ina asilimia 61.3 ya wanawake bungeni, kielelezo cha ushirikishwaji na usawa.
Lakini katika bara la nchi 54, kwa nini ni nchi chache zinazoongozwa na wanawake?
Na hapa ndipo mjadala unapoibuka:
Vizuizi vya kitamaduni
Tamaduni nyingi barani Afrika bado zinaamini kuwa wanawake hawapaswi kuwaongoza wanaume.
Ingawa katika sehemu nyingi dhana hii potovu imesambaratishwa na kufutwa, bado ni jambo linalojitokeza kila kukicha, japo sio kwa kutamkwa wazi, vitendo vinaeleza.
''Watu wanasema wanawake hawajitokezi kuchaguliwa, lakini hata hivyo tunajitahidi sana, hata kama tunafanya kampeni na tumehitimu zaidi, watu huchagua tu wanaume, bila sababu ya msingi …'' anasema Anne Waithera, mgombea ubunge kutoka Kenya.
Amegombea nafasi hiyo mara mbili lakini hajawahi kushinda.
‘’Wakati mwingine ninahisi wanawake wenzetu wanaharibu nafasi zetu wenyewe, na wanakataa kutupigia kura,’’ anaongeza.
Nadharia ya iwapo wanawake ni maadui wao wenyewe imeenea sana nchini Kenya na maeneo mengine ya Afrika Mashariki katika siku za hivi karibuni, hasa baada ya uchaguzi.
Mojawapo ya dhana ni kwamba wanawake wako radhi kuongozwa na mwanamume fidhuli kuliko kumuona mwanamke mwenzao akiwa madarakani.
Lakini uchunguzi wa jarida la Forbes mnamo 2023 ulionyesha kuwa wanawake ni viongozi sawa na wanaume au hata bora zaidi.
‘’Kwa mara ya kwanza katika historia, Wakurugenzi Wakuu wanawake wanaongoza takriban 10% ya kampuni 500 kubwa zaidi . Hii bila shaka ni hatua muhimu. Lakini pia inasisitiza haja ya wanawake zaidi katika ngazi zote za uongozi,’’ ulisema utafiti huo.
Na hii sio tu juu ya uwakilishi. Utafiti umeonyesha kuwa baadhi ya viongozi wanawake ni wazuri katika biashara.
Wanawake zaidi ya siasa
Katika kupigania haki ya kijamii na kimazingira, wanawake wa Kiafrika wamethibitisha uwezo wao wa uongozi.
Askari wa Akashinga Rangers nchini Zimbabwe, ambao ni kitengo cha wanawake pekee cha kupambana na ujangili, sio tu wanalinda wanyamapori lakini wanabadilisha jamii kupitia uwezeshaji.
Katika biashara, majina kama Ngozi Okonjo-Iweala wa Nigeria, ambaye anahudumu kama Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Biashara Duniani, anaonyesha nguvu ya wanawake katika uongozi wa kiuchumi duniani.
Wanawake wengi wa Kiafrika wanaongoza mipango inayoshughulikia huduma za afya, elimu na kupunguza umaskini.
Wanawake hawa wanathibitisha kuwa uongozi hauishii kwenye ofisi za juu tu bali hustawi katika kiini cha jamii.
Wasichana wengi wanapoingizwa madarasani barani Afrika, na kupewa nafasi na sauti kusikika, wanawake zaidi hupata nguvu ya kupiga hatua na kuonyesha umahiri wao.
Msemo wa zamani kwamba nyuma ya kila mwanamume aliyefanikiwa, anasimama mwanamke mwenye nguvu, huenda usiwe na maana tena, kwa sababu kwa kadri wanawake wanaounga mkono wanavyothaminiwa, wanahitaji kujua kwamba jukumu lao sio kushangilia tu, wanaweza pia kuchagua kunyakua mwenge na kukimbia nao.