Na Coletta Wanjohi
Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa sasa ina nchi nane wanachama. Ilianzishwa 1967 na nchi 3 za msingi ambazo ni Tanzania, Kenya na Uganda. Lakini mwaka 1977 Jumuia hiyo Ikavunjwa.
November 30, 1999, nchi hizi kwa mara nyengine, zilifanya makubaliano ya kisheria ya kuunda Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo baada ya muda, ilivutia nchi nyengine kutaka kujiunga.
Nchi hizo ni pamoja na Rwanda, Burundi, Sudan Kusini, Jahmuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na Somalia. Kujiunga kwa nchi hizo, ni fursa ya kuleta rasilimali kwa manufaa ya kikanda, hivyo kuifanya Jumuia hiyo hivi sasa, kuwa na jumla ya idadi ya watu milioni 300 kutoka nchi wanachama.
Hili ni soko katika ukanda wa Afrika Mashariki na iwapo litatumiwa vizuri basi linaweza kuinua uchumi wa nchi husika hasa kibiashara.
Ni mantiki hiyo, ambapo nchi wanachama zimekubali kuanzisha biashara huria kati yao ambapo hakutakuwa na ushuru kwa bidhaa na huduma miongoni mwao na kukubaliana juu ya ushuru wa pamoja wa nje.
Miongoni mwa faida za Jumuia hiyo ni pamoja na raia wa nchi wanachama kuruhusiwa kuingia nchi nyengine bila kuzingatia masharti ya viza huku baadhi ya nchi zikiondoa ada za vibali vya kufanya kazi.
Mwaka 2016 hati ya kusafiria ya kielektroniki ya Afrika Mashariki ilizinduliwa ikilenga kurahisisha raia wake kusafiri ndani ya jumuiya.
Huku nchi mpya zikiendelea kujiunga, mikakati ya kuhakikisha manufaa haya yanasambaa kwa usawa kwa nchi zote inaendelea, kukiwa na nia ya kuunda umoja wa kisiasa.
Na kadri ambavyo nchi wanachama zinaingia katika jumuiya na kuleta manufaa yao, lakini ndivyo hivyo zinaleta changamoto katika Jumuia.
Amani na usalama
Sudan Kusini licha ya kuleta manufaa ya kiuchumi ya mafuta, bado ina changamoto ya kujikwamua kutoka kwa athari ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoanza 2013 hadi 2018 wakati makubaliano ya amani yalipofanyika.
Somalia ambayo ndio mwananchama mpya wa hivi karibuni, imengia na changamoto ya usalama dhidi ya kikundi cha Al Shabaab, hivyo hii sasa inalazimika kuwa ajenda ya Jumuiya.
Katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC vita kati ya serikalli na waasi wa M23 vimeleta mvutano katika Jumuiya ya EAC.
Kwa moyo ya kutoa usaidizi kwa mwanachama wao mpya DRC, Jumuiya ya EAC iliamua mwaka 2022 kutuma kikosi cha kuleta amani nchini humo.
Hata hivyo, mwaka mmoja baadaye, DRC ilikataa kuongeza muda wa kikosi hicho cha Afrika Mashariki ikidai kuwa hakitimizi malengo yake ipasavyo.
Pia kumekuwa na uhasama wa kidiplomasia kati ya DRC na Rwanda ambao wote ni wanachama wa EAC, huku DRC ikiilaumu Rwanda kwa kuungana na waasi wa M23.
Rwanda na Burundi nazo zina mvutano wa kidiplomasia. Burundi imekuwa ikiilaumu Rwanda kuwa inafadhili na kutoa mafunzo kwa waasi wa kundi la RED-Tabara.
Rwanda siku zote imekuwa ikikana tuhuma hizo.
Mivutano hii inaathiri umoja na maendeleo ya jumuiya kwani hata marais wa nchi hizi kukutana pamoja katika mikutano muhimu ya Jumuiya imekuwa vigumu.
Hata hivyo, Jumuiya ya Afrika Mashariki ina amini kwamba, kupitia vyombo vyake vya umoja vya kisiasa, kiuchumi na kijamii, bado manufaa ya umoja yataonekana.