Vita vya Israel dhidi ya Gaza vimesababisha vifo vya takriban Wapalestina 39,623 na kuwajeruhi wengine karibu100,000. /Picha: AFP

Na Nuri Aden

Kitivo cha Sheria katika Chuo Kikuu cha Istanbul cha Boğaziçi kiliandaa kongamano la siku mbili mwishoni mwa juma lililopita, ambalo liliwaleta pamoja zaidi ya wataalam 100 wakuu wa sheria duniani ili kufikiria upya mfumo thabiti zaidi wa kisheria wa kimataifa katika muktadha wa mauaji ya kimbari ya Israeli huko Gaza.

Na'eem Jeenah, mwandishi na mtafiti mkuu katika Taasisi ya Mapungubwe Institute for Strategic Reflection ya Afrika Kusini, aliwasilisha mada kwa ufasaha kuhusu suala la Palestina kama sehemu wa kile alichokiita "mchakato wa Afrika wa kuondoa ukoloni".

"Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu imetoa taarifa maalum kuhusu suala la Palestina na Umoja wa Afrika kuwa dhidi ya Uzayuni na kutaka kuondoa ushawishi wa Kizayuni kutoka Afrika," aliiambia TRT Afrika pembezoni mwa semina iliofanyika Agosti 3-4, ilioangazia mada ya "Kufikiria tena Sheria ya Kimataifa baada ya Gaza".

Utetezi wa Jeenah unaakisi mpango wa Afrika Kusini wa kuakilisha kesi mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) mnamo Desemba 29 mwaka jana kuhusu mauaji ya kimbari ya Israeli dhidi ya Wapalestina huko Gaza. Israeli imewauwa takriban Wapalestina 40,000 huko Gaza tangu Oktoba mwaka jana.

Mafunzo kwa siku zijazo

Jaji mstaafu wa Mahakama Kuu ya Magharibi mwa Cape Siraj Desai, ambaye anaongoza Ombud Afrika Kusini, alielezea haja ya ushirikiano wa kisheria kuchukua hatua kwa ajili ya Gaza huku akiunda ajenda za baadaye za kisheria na kisiasa.

"Mkusanyiko huu wa kisheria, wa kielimu unachangia katika kujenga utaratibu mpya wa kisheria na unaelekeza ajenda ya kisiasa na kisheria kwa miaka ijayo sio tu kwa Palestina bali kwa ulimwengu wote katika siku zijazo," alisema.

Nchi nyingi kama vile Uturuki zimeunga mkono kesi ya mauaji ya halaiki ya Afrika Kusini dhidi ya Israeli katika mahakama ya ICJ.

''Hii inaongeza uzito katika kesi iliyo mbele ya ICJ kwamba Palestina sasa ni taifa linalotawaliwa na koloni," aliongeza.

Richard Falk, ripota maalum wa zamani wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu, alitoa mtazamo wake katika mazungumzo juu ya "Changamoto ya Gaza: Je, sheria ya kimataifa ni muhimu ikiwa haiwezi kutekelezwa?"

Afrika Kusini iliishutumu Israeli kwa kufanya mauaji ya halaiki huko Gaza mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki. /Picha: Reuters

Anajua, baada ya kufukuzwa na Israeli wakati wa mchakato wa kuripoti ukiukaji wa haki za binadamu huko Gaza.

Michael Lynk, ripota mwingine maalum wa zamani wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu, alizungumzia uharamu wa walowezi wa Israeli katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na vitendo vya ubaguzi wa rangi zinazokiuka Mkataba wa Roma wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai.

Umuhimu mkubwa wa Mada kama vile "Haki kwa Palestina na Uwezo wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki", "Sheria ya Kimataifa ya Kibinadamu: Ufikiaji, Haki, Nafasi za Kidijitali, na Mustakbali", na "Haki za Kijamii na Kiuchumi katika Maeneo Yanayokaliwa ya Palestina" mazungumzo juu ya kurekebisha sheria za kimataifa ili kuhakikisha kuwa inahudumia mataifa yote kwa usawa, kwa kuzingatia uhalifu dhidi ya ubinadamu huko Gaza.

"Waafrika Kusini wengi wanalaani mauaji ya halaiki kwa sababu watu wa Afrika Kusini wanajua kuwa haya ni mauaji ya halaiki na shambulio lisilozuilika dhidi ya Wapalestina," Desai alisema.

Everisto Banyera, profesa katika Chuo Kikuu cha Afrika Kusini, alisema ni wakati muafaka wa mfumo wa sheria wa kimataifa kurekebishwa kwa kushirikisha washikadau wote "ili uweze kufanya kazi kwa haki kwa ajili yetu sote".

Kulingana na yeye, hatua ya kuanzia itakuwa kutupilia mbali wazo kwamba hii ni matamanio tu.

"Hatuwezi kuendelea kuwa na hali ambapo wachache waliobahatika kubuni na kulazimisha ujuzi wao, uzoefu, na uwezo wao wa kisheria katika mfumo wa sheria za kimataifa, ambazo zinatufunga sisi sote. Iwapo itakuwa sheria inayotufunga sote, basi lazima tuhusishe na tuwakilishe maoni ya kila mtu katika maandalizi yake," Banyera alisema.

'Afrika haiko huru hadi Palestina iwe huru'

Aliashiria kuongezeka kwa mshikamano wa kimataifa na kadhia ya Palestina kama mfano wa uhakika.

Jeenah, ambaye aliwasilisha kikao cha "Kuweka upya Sheria ya Kimataifa: Mielekeo na Changamoto za Kimataifa za nchi Zinazoendelea", alisema matatizo ya Palestina yanapaswa kuchukuliwa kama sehemu ya sababu pana ya kukomesha ukoloni.

"Afrika ina jukumu la kukomesha mchakato huo," alisema. "Mchakato wa Afrika wa kuondoa ukoloni haujaisha hadi pale Palestina iwe huru, na mapambano ya Wapalestina ni mapambano ya Afrika.

"Mtafiti mkuu aliangazia kuhusu "uhusiano wa karibu" wa kihistoria kati ya vuguvugu la ukombozi wa Kiafrika na mapambano ya Wapalestina kama kielelezo cha kuendelea kuunga mkono watu wenye subira wa Gaza.

Jeenah alionyesha wasiwasi wake kwamba kushindwa kukomesha mauaji ya kimbari ya Israeli huko Gaza kutatia moyo mataifa mengine wavamizi duniani kote, na nchi za Kiafrika zinaweza kukumbwa na matokeo hayo.

"Suala la Palestina ni kiashiria cha mapambano ya siku zijazo kati ya nchi maskini na zinazoendelea, ikiwa ni pamoja na mataifa ya Afrika, na nchi zenye nguvu zilizoendelea," Jeenah alisema.

"Tunataka kuona ulimwengu unaosifika kwa haki za binadamu na haki bora za kijamii na kiuchumi kwa watu waliotengwa."

Wazungumzaji wengine katika kongamano hilo ni pamoja na Balakrishnan Rajagopal, ripota maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya makazi mazuri, na Hilal Elver, ripota maalum wa zamani wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya kupata chakula.

Wamelaani kuendelea kushambuliwa kwa Gaza na Israeli na kueleza kusikitishwa na mateso ya Wapalestina.

TRT Afrika