Tarehe 23 Agosti, ni siku ya kimataifa ya kukumbuka Biashara ya Utumwa na kukomeshwa kwake./ Picha: UNESCO

Na Dayo Yussuf

TRT Afrika, Istanbul

Wanasaikolojia wanasema ni kawaida kwa akili kutaka kuzuia na kupotezea matukio mabaya au kumbukumbu mbaya.

Katika hali nyingi ni aina ya utaratibu wa kukabiliana na kiwewe ambacho watu hutumia kujaribu na kuendelea na maisha.

Lakini hii inaonekana kuwa sivyo linapokuja suala la biashara ya watumwa.

Watu wengi humulika historia ya biashara hii ya zamani kwa mitazamo tofauti, wengine wanashangaa wasijue wapokee vipi.

Hakika huleta hisia mchanganyiko kulingana na upande upi unaoutazama. Wale ambao walinufaika lakini wanajuta wanataka kuficha nyuso zao kwa aibu, wakati wale ambao mababu zao walipigana kuiondoa watataka kukumbuka juhudi hizo kwa fahari.

Lakini zaidi ya karne mbili zimepita tangu biashara hiyo kukomeshwa duniani kote, angalau rasmi kwenye mkataba, hivyo kwa nini kuitaja tu biashara ya utumwa bado kunaacha ladha chungu kwa vizazi vya sasa.

Wataalamu wa historia wanasema hii mara nyingi hutokana na wahusika walikuwa ni kina nani, na jinsi vizazi vyao vinawakumbuka.

''Kumbukumbu ya biashara ya utumwa inakua kulingana na wafanyabiashara, serikali walikotoka wafanyabiashara hao, wapokeaji wa watumwa hawa, na wanufaika wa biashara hiyo,'' anasema David Kyule, mhadhiri wa idara ya Historia na Akiolojia katika Chuo Kikuu cha Nairobi. Ukiuliza nchi kama Uingereza au Brazil na Marekani, baadhi watakumbuka kwa matamanio, wengine watatafakari na kadhalika,’’ Bw Kyule aliambia TRT Afrika.

Kwa hivyo ni wazi sisi sote hatukumbuki biashara ya watumwa kwa njia sawa.

Kwa hivyo kwa nini ni muhimu sana kukumbuka?

Mabishano juu ya kile kinachopaswa kukumbukwa kuhusu utumwa yamejikita sana katika jinsi historia inavyofundishwa. /Picha: UNESCO

Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni liliona ni muhimu sana kutenga siku kwa ajili ya kumbukumbu hiyo.

Tarehe 23 Agosti, ni siku ya kimataifa ya kukumbuka Biashara ya Utumwa na kukomeshwa kwake.

Kulingana na UNESCO, siku hii mnamo 1791 Jamhuri ya Haiti, iliona mwanzo wa maasi ambayo yangechukua jukumu muhimu katika kukomesha biashara ya utumwa ya kuvukisha Atlantiki.

Na kufikia mwanzoni mwa karne iliyofuata, nchi kama Uingereza zilitekeleza mikataba ya kukomesha biashara hiyo.

''Siku hii ya Kimataifa inakusudiwa kuweka janga la biashara ya utumwa katika kumbukumbu ya watu wote…..inapaswa kutoa fursa ya kuzingatia kwa pamoja sababu za kihistoria, mbinu na matokeo ya janga hili,'' ilisema sehemu ya taarifa ya Mkurugenzi wa UNESCO kwenye tovuti yao.

Mitaala inaficha ukweli

‘’Unapozungumzia kukumbuka biashara ya utumwa, unahitaji kujiuliza, ni nini unataka kukumbuka, na ni kwa umbali gani unataka kukumbuka?’’ anauliza Bw Kyule. ‘’Watu wanazungumza tu kuhusu Afrika lakini hii, inaishia wapi na inaanzia wapi? Tuna utumwa wa tangu enzi za biblia, utaupata pia katika Qur'an, na hii ilikuwa tofauti na utumwa wa Wafaransa, Waingereza au Wahispania,’’ anaongeza.

Lakini mabishano juu ya kile kinachopaswa kukumbukwa kuhusu utumwa yamejikita sana katika jinsi historia inavyofundishwa.

Kumekuwa na kilio kikubwa hasa kwa nchi za Magharibi juu ya kile 'wanachoficha' kwenye vitabu vyao vya historia au wakati mwingine hata kupindisha ukweli ili kuepuka kuaibishwa au kuwajibika kwa uhalifu wa baba zao. Uhalifu ambao bado wanaendelea kufaidika nao.

‘’Ni swali la mtindo gani wa historia unataka ufundishwe,’’ asema Bw Kyule. ‘’Kwa mfano waliofanya biashara ya utumwa watakuwa na simulizi yao wenyewe ya jinsi ilivyokuwa, na watumwa wenyewe wangekuwa na simulizi yao ya jinsi ilivyo. Waliochangia, kama vile Kanisa Katoliki, kwa mfano ambao walishiriki jukumu kubwa sana katika utumwa huko DRC, watasema nini kuhusu hilo? Wengi hupotosha historia ili kuendana na simulizi yao au serikali zao,’’ anaongeza.

Biashara ya Utumwa ya Atlantiki huenda ndiyo iliyokuwa ghali zaidi katika maisha ya binadamu kati ya uhamiaji wote wa masafa marefu duniani./ Picha: TRT Afrika

Jukumu la kupata historia sahihi ya utumwa si la waliofaidi tu, bali hata waathirika.

Kuna historia kubwa ya jinsi baadhi ya viongozi wa Kiafrika wa wakati huo walivyohusika katika biashara hiyo, au kunufaika nayo moja kwa moja. Haikuwa kitu cha ajabu kwa mfano kuona baadhi ya machifu wa Kiafrika wakifanya kazi na wafanyabiashara wa Kiarabu kuuza watumwa.

Athari za biashara ya watumwa

Mwanahistoria Bw Kyule anasema wakati wa kukumbuka Biashara ya Utumwa, ni muhimu pia kuiangalia kutoka pande zote na wadau katika biashara hiyo na jinsi walivyoathiriwa. Sio kubadilisha hadithi, ni kulenga kusimulia hadithi ya kweli.

''Ili kupata ukweli juu ya biashara ya utumwa, tunahitaji kujua ilikua na jukumu gani hasa katika maendeleo ya uchumi wa dunia ya kisasa. Tunazungumza kuhusu mabenki, kama Barclays ambayo ilianzishwa kutokana na mapato ya moja kwa moja ya biashara ya utumwa. Tunazungumzia mataifa yaliyoundwa au kujiendeleza kupitia biashara ya utumwa, hayo ndiyo mambo tunayohitaji kuyafikiria pia,’’ anaiambia TRT Afrika.

Katika kipindi cha Biashara ya Utumwa ya Atlantiki, kuanzia takriban 1526 hadi 1867, wanaume, wanawake, na watoto wapatao milioni 12.5 waliotekwa waliwekwa kwenye meli barani Afrika, na milioni 10.7 walifika Amerika.

Biashara ya Utumwa ya Atlantiki huenda ndiyo iliyokuwa ghali zaidi katika maisha ya binadamu kati ya uhamiaji wote wa masafa marefu duniani.

Utumwa chini ya jina jipya

Lakini tarehe 23 Agosti sio tu kuhusu ukumbusho bali pia kuashiria kukomeshwa kwa biashara ya utumwa.

Na huwezi kutenganisha mambo hayo mawili sababu ikiwa kumbukumbu ya uhalifu itapotoshwa, unawezaje kukiri juhudi za kuurekebisha?

Katika kipindi cha Biashara ya Utumwa ya Atlantiki, kuanzia takriban 1526 hadi 1867, wanaume, wanawake, na watoto wapatao milioni 12.5 waliuzwa kama watumwa nchini Marekani,/ Picha : Getty

Kwa bahati mbaya, wengi wanaamini kwamba utumwa uliwekwa kwa sura mpya na kuuzwa kwa ulimwengu, mara nyingi ukiwa umefichwa mbele ya macho yetu.

‘’Kama vile ukoloni, tunaambiwa kwamba tulipata uhuru, lakini je, ni kweli tulipata uhuru huo,’’ Bw Kyule anauliza. ‘’Kwa hiyo hapana! Utumwa haukuisha pia. Wahusika walikubali haraka kuwa kama biashara, utumwa wa wazi haukuwa endelevu, hivyo kulazimika kubadili mtindo ili waendelee na biashara kisiri,’’ anasema.

Kulingana na wataalamu, ukoloni ulifanywa kuwa wa kisasa (Ukoloni Mambo leo) na kupitishwa kwa mawakala wa wakoloni ambao walikuwa tayari kufanya kampeni za mabwana wao kwa gharama ya nchi zao.

Hili lilifanyika kwa ujanja kwa kupitisha katiba zile zile za kikoloni ambazo katika baadhi ya nchi za Afrika bado zinatumika. Baadhi ya wakoloni kama Waingereza na Wafaransa waliacha mitaala ya shule ambayo ilipaswa kufundishwa kwa vijana wa Kiafrika, mifumo ya uongozi na dini, na kadhalika.

Na ndivyo hali ilivyokuwa pia na Utumwa.

Africa slavery

‘’Sioni tofauti kati ya ukoloni na mabadiliko ya sura ya biashara ya watumwa na utumwa,’’ Bw Kyule asema. ‘’Kwa mfano kwa maoni yangu, Usafirishaji Haramu wa Binadamu ni neno jengine la kuvutia la Biashara ya Utumwa. Kazi ya kulazimishwa bado ipo katika maeneo mengi, kuanzia majumbani mwetu na wafanyakazi wa nyumbani,’’ anaiambia TRT Afrika.

Wataalamu wanasema si lazima uangalie mbali ili kuona dalili za utumwa wa kisasa.

Kusafirisha wafanyakazi wa ndani hadi nchi za Kiarabu licha ya ripoti nyingi za unyanyasaji. Kukiuka haki za wafanyakazi na kuwanyang'anya vitambulisho na pasipoti zao, kuwakataza kujiunga na vyama vya wafanyakazi, au kuwanyima malipo, siku za kupumzika au kuamuru jinsi wanavyotumia siku zao za mapumziko na kadhalika.

Orodha haina mwisho lakini hutokea kila siku mbele ya macho yetu.

TRT Afrika