Korea Kusini ilipokea wajumbe kutoka nchi 48 za Afrika, karibia 25 kati yao wakiwa viongozi wa nchi na serikali. Picha: Ikulu ya Nairobi.

Na

Sylvia Chebet

Mwanauchumi wa Kenya XN Iraki anachambua suala la kumezewa mate Afrika kutumuia taaluma yake.

"Afrika ni kama msichana mrembo; kila mwanamume anataka mkono wake," Iraki amesema, akirejea kutoka mkutano wa kilele wa kati ya Korea Kusini na Afrika, uliomalizika hivi majuzi, mkutano huo ulihudhuriwa na wakuu 25 wa nchi na serikali katika mji wa Ilsan na Seoul.

Mkutano wa Juni 4-5 lilikuwa ni moja ya mfululizo wa mikutano ya kilele ya Afrika iliyoandaliwa na Urusi, Italia, China na Ufaransa.

Kama wachumba wengine wa Afrika, Seoul imeahidi uwekezaji wa mabilioni ya dola kwa bara hilo.

"Ili kuongeza ushirikiano na Afrika, Korea Kusini itaongeza ODA (Mpango Rasmi wa Usaidizi wa Maendeleo) hadi kufikia dola bilioni 10 za Marekani ifikapo 2030," Rais Yoon Suk Yeol alitangaza kwenye mkutano huo.

"Korea Kusini pia itatoa dola bilioni 14 katika ufadhili wa mauzo ya nje," alisema.

Kulingana na Iraki, profesa katika Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Nairobi, yeyote anayekanusha kumezewa mate kwa Afrika ni aidha" amelala au anasinzia."

Ukisinzia utapoteza

Marekani ilionekana kujificha baada ya Mkutano wake wa Kilele wa Afrika wa 2014, na kupoteza nafasi ya kiuchumi kwa China na kwa Urusi katika nyanja ya usalama.

Rais Joe Biden na Rais William Ruto wakitembea na wake zao kuingia Ikulu ya White House kwa chakula cha jioni, Mei 24, 2024. Photo: Ikulu ya Nairobi

Lakini mwezi huu wa Mei, Washington imetandika zulia jekundu kwa Rais William Ruto wa Kenya. Chakula cha jioni cha White House wakati wa ziara hiyo kilikuwa cha kwanza kwa kiongozi wa Afrika baada ya miaka 15.

"Tunazindua kile tunachoita maono ya Nairobi-Washington," Rais Joe Biden alisema wakati wa mkutano wa pamoja na Ruto katika Ikulu ya White House.

"Mpango huu utaleta pamoja taasisi za fedha za kimataifa ili kukusanya rasilimali zaidi kwa nchi zilizojaa madeni, kufungua fursa zaidi za ufadhili wa sekta binafsi, na kuleta uwazi zaidi, uendelevu na mbinu nafuu za kukopesha."

Kwa upande wake, Rais Ruto alisema kwa uwazi kuwa nchi hiyo ya Afrika Mashariki hailekei upande wa Mashariki wala ule wa Magharibi lakini unaangalia "mbele." Alisema Marekani ilikuwa na fursa ya kurekebisha kwa kiasi kikubwa ushawishi wake barani Afrika.

"Amerika inahitaji kujitokeza," Ruto alisema. "Kuwa na demokrasia, kuwa nchi inayoamini katika utawala wa sheria. Demokrasia lazima ipatikane."

Wataalamu wa mambo waliona hili kama kukiri kwamba Marekani ilikuwa imerudi nyuma na ilihitaji kushika kasi.

Katika kuonyesha kasi mpya, Biden alitangaza mpango wa Congress kuteua Kenya kama mshirika mkuu asiyekuwa mjumbe wa NATO.

Sababu ya zawadi ya NATO

Likiwa limeundwa kukabiliana na Umoja wa Kisovieti wa zamani na washirika wake, Shirika la Mkataba wa Atlantiki ya Kaskazini (NATO) limekuwepo kwa miaka 75. Madhumuni yake ni kuhakikisha usalama na uhuru kwa nchi za Ulaya na Amerika Kaskazini katika ncha zote mbili za Bahari ya Atlantiki kupitia rasilimali zake za kisiasa na kijeshi.

"Kwa hiyo, kuwa mshirika asiyekuwa mjumbe wa NATO inamaanisha kuwa unaweza kufikia baadhi ya vifaa vya kijeshi, programu na kijasusi, kwa matumaini kukufanya kuwa nchi salama zaidi," Iraki anaiambia TRT Afrika. "Lakini unaweza usipate ulinzi mwingi kama mwanachama wa NATO, kama vile kusaidiwa ikiwa unashambuliwa."

Anasema tangu kupokea hadhi ya kuwa mshirika mkuu asiyekuwa mjumbe wa NATO, mataifa matatu ya Afrika - Morocco, Tunisia na Misri yamefaidika na vifaa vya kijeshi na sasa yanahesabiwa kuwa miongoni mwa majeshi yenye nguvu zaidi katika eneo la Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika.

Kenya itakuwa nchi ya kwanza kusini mwa jangwa la Sahara, na taifa la 19 kuteuliwa kuwa mshirika mkuu asiye kuwa mjumbe wa NATO. Picha: Ikulu ya Nairobi

Pindi Bunge la Marekani litakapoidhinisha, Kenya itakuwa nchi ya 19 kutajwa kuwa mshirika mkuu asiyekuwa mjumbe wa NATO, na ya kwanza katika ukanda wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Lakini kuna upande mwingine wa suala hili. "Nina hofu kwamba kwa kuonyesha wazi mshikamano wetu (wa Kenya) na Marekani, tunaunda maadui wapya. Swali kuu ni ikiwa manufaa yatazidi hasara," anasema Iraki.

Mwanauchumi na mtoa maoni pia anaibua wasiwasi mwingine. "Kenya pengine inavunja hadhi yake ya kutoegemea upande wowote kwa kuwa mshirika asiyekuwa mjumbe wa NATO."

Hata hivyo, wachambuzi wengi wanaamini kwamba suala la kutoegemea upande wowote umepitwa na wakati, katika ulimwengu unaozidi kuwa wa mabingwa wengi. Sasa, nchi zinatafuta miungano inayohudumia maslahi yao.

Hakuna chakula cha bure

Marekani inaihesabu Kenya miongoni mwa washirika wake thabiti wa kidemokrasia katika bara hilo, ikithamini mchango wake katika juhudi za amani na usalama katika nchi zenye matatizo kama vile Somalia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Sudan na Haiti.

Ingawa ushirikiano huu wa kimkakati umedumu kwa miaka 16, wachambuzi wameliangalia zaidi kuhusu wema wa hivi majuzi wa Marekani kwa Nairobi. Ushawishi wa Marekani barani Afrika umefifia katika kipindi cha miaka 50 iliyopita na inachukua fursa hiyo kurejea tena.

"Nadhani Marekani pia inasema hatuwezi kuacha rasilimali za Afrika kwa China pekee. Inataka hisa kubwa," anasema Iraki.

Rais Ruto alirejea nyumbani kutoka kwa ziara yake ya kiserikali ya siku tatu akiwa na mambo mengi mazuri, ikiwa ni pamoja na mradi wa barabara ya mwendokasi wa Nairobi-Mombasa wenye thamani ya dola bilioni 3.5 na mkataba wa usalama wa dola bilioni 7.

Marekani pia inatuma helikopta 16 na takriban magari 150 ya kivita ili kuimarisha ushiriki wa Kenya katika misheni za kulinda amani.

Baadhi ya wachambuzi wanatabiri kuwa nchi za Mashariki huenda zikajibu kwa ofa kubwa zaidi za biashara na uwekezaji ili kukabiliana na Marekani.

"Tunatumai kwamba tutafaidika kutoka Mashariki na Magharibi kwa muda mrefu. Kama wanavyosema kwa Kiswahili, tutapita kati yao (tutapita katikati)," anasema Iraki.

Kufafanua maslahi

Kulingana na kasi mpya ya ukuaji, wataalam wanapendekeza kwamba bara lenye nguvu zaidi ulimwenguni linahitaji kufafanua masilahi yake ya kimkakati kwa uwazi ili kupata faida endelevu kutoka kwa hazina yake ya madini.

"Nina hakika umegundua kuwa siku hizi wanandoa wana makubaliano kabla ya kufunga ndoa," anasema Iraki. "Ikiwa hatuna masilahi yaliyoainishwa vizuri, tutachezewa."

Mwanauchumi anasisitiza kwamba wananchi wa kawaida walio chini kabisa ya piramidi wanapaswa kuhisi athari za ushirikiano au miungano hii kwanza kabisa.

"Mwisho wa siku, watu wanataka pesa mifukoni mwao, iwe serikali zao zinaelekea Mashariki au Magharibi," anasema. "Lazima iwe hadithi ya ukuaji wa uchumi wa pande zote. Ushindi wa kila mtu."

TRT Afrika