Africa food Summit in Tanzania

MKUTANO wa 13 wa Jukwaa la Mifumo ya chakula barani Afrika umeanza leo jijini Dar es salaam Tanzania.

Mkutano huo unawakutanisha washiriki zaidi ya 4000 kutoka kote ulimwenguni miongoni mwao wakiwa viongozi na wavumbuzi kujadili sera, mafanikio na ubunifu katika kilimo pamoja na mabadiliko ya mifumo ya chakula.

Kilimo ni mojawapo ya sekta zilizoathirika zaidi duniani huku ikikabiliwa na changamoto kama mabadiliko ya hali ya hewa, mabadiliko ya mifumo ya matumizi, ukuaji wa idadi ya watu, upotevu wa baioanuai, uchafuzi wa mazingira, migogoro, uhamiaji, na migogoro na mivutano ya nje ya Afrika.

''Afrika itakuwa na zaidi ya asilimia 40 ya vijana katika nchi za kipato cha chini na cha kati ifikapo mwaka 2050,'' imesema Benki ya Dunia katika ripoti yake. '' Mikakati thabiti inahitajika kuhakikisha mahitaji ya msingi ikiwemo chakula vinakuwa vya uhakika,'' ripoti hiyo imeongezea.

Mikakati thabiti inahitajika kuhakikisha mahitaji ya msingi ikiwemo chakula vinakuwa vya uhakika/ Picha : Wizara ya Kilimo Tanzania 

Kwa mantiki hii wadau wa masuala ya maendeleo wanaeleza kuwa ipo haja kujipanga kwa kuhakikisha mifumo ya chakula inaendelea kywa thabiti.

Kwa upande wake Benki ya ya Maendeleo ya Afrika AFDB inasema, '' Ifikapo mwaka 2063, Afrika itasalia kuwa eneo changa zaidi duniani, likiwa na umri wa wastani wa miaka 25, tafakuri ya kina kuhusu nguvu kazi hii katika uzalishaji wenye tija hasa wa chakula inapaswa kupewa uzito mkubwa,''

Amath Pathe Sene, Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula barani Afrika, ameeeleza kuwa ipo haja kubwa ya kukabiliana na changamoto za mfumo wa chakula, akisisitiza kwamba ni muhimu Afrika isikike na kuendeleza ufumbuzi kulingana na changamoto husika za Bara la Afrika huku vijana na wanawake wakibebwa katika kila hatua za kubadilisha mifumo ya Chakula.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan atawaongoza Viongozi wa Mataifa ya Afrika takriban 15 na wengine wa mashirika ya kimataifa pamoja na washiriki kutoka mataifa zaidi ya 100 katika mkutano huu wa siku nne ambapo mijadala mbalimbali itashika hatamu ikiongozwa na kauli mbiu ya mkutano huu ya ‘kuhuisha, kuweka mikakati mipya na kuchukua hatua’

TRT Afrika