Raia wa Msumbiji wapatao milioni 5.3 wanatarajia kupiga kura Oktoba 9, 2024 kumchagua rais mpya wa nchi hiyo.
Rais anayemaliza muda wake, Filipe Nyusi, kutoka chama cha FRELIMO, hatogombea tena nafasi hiyo baada ya kuhudumu kwa mihula miwili.
Tayari vyama kadhaa vya upinzani nchini humo vimeweka wagombea wake watakaoshindana katika uchaguzi huo. Ifuatayo ni orodha na wasifu wa wagombea urais watakaoshiriki mchakato huo.
Daniel Chapo
Huyu ni mgombea mwenye umri wa miaka 47, na atawania uongozi wa nchi hiyo kupitia tiketi ya chama tawala cha Frelimo cha nchini Msumbiji. Frelimo kimekuwa madarakani tangu uhuru wa nchi hiyo wa mwaka 1975.
Chapo anapigiwa chapuo kushinda uchaguzi wa Oktoba 9 kutokana na umaarufu wa chama chake, ingawa yeye mwenyewe sio maarufu sana. Amewahi kuwa mtangazaji wa redio na kufundisha sheria katika ngazi ya Chuo Kikuu. Aliingia rasmi kwenye siasa mwaka 2009, na miaka ya hivi karibuni amewahi kuwa gavana wa mkoa wa kusini wa Inhambane.
Ossufo Momade
Ossufo Momade, mwenye umri wa miaka 63, ni kiongozi wa chama kikuu cha upinzani ambacho pia kiliwahi kuwa vuguvugu ya waasi, Renamo. Pia aliwahi kugombea Urais katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2019 na kuibuka wa pili kwa asilimia 22 ya kura, ingawa chama chake kilidai kuibiwa kura na kupinga matokeo mahakamani. Momade alikuwa ni Jenerali Renamo katika vita na Frelimo vilivyodumu kwa miaka 16 ambavyo vilisitishwa 1992. Mapigano yaliendelea baada ya vita mpaka Momade na Nyusi waliposaini makubaliano kwa niaba ya vyama vyao mwaka 2019.
Venancio Mondlane
Mgombea binafsi Venancio Mondlane anaonekana kama nyota inayochomoza katika siasa za Msumbiji kwa kuwa ana haiba kubwa miongoni mwa vijana.
Mondlane alikuwa mwanachama wa Renamo mpaka alipotoka mwaka huu ili agombee urais kwa msaada wa chama chengine cha Democratic Alliance Coalition (CAD).
Hata hivyo, Baraza la Katiba la Msumbuji, mwezi Agosti lilifuta usajili wa chama hicho, Mondlane akibaki kuwa mgombea binafsi.
Wachambuzi wa siasa wanasema kwamba, Mondlane ni tishio kubwa kwa Frelimo, lakini kukosa uungwaji wa chama kunaweza kudhoofisha nafasi yake.
Mwaka jana, mwanasiasa huyo, alishindana na mgombea wa Renamo katika nafasi ya umeya kwa jiji la Maputo na alidai kushinda, lakini mgombea wa Frelimo alitangazwa mshindi huku kukiwa na tuhuma za wizi wa kura, Frelimo ilikana madai hayo.
Lutero Simango
Lutero Simango ni kiongozi wa chama cha Mozambique Democratic Movement (MDM), chama cha tatu kwa ukubwa nchini humo, ambacho mwanzilishi wake alikuwa kaka yake Daviz Simango mwaka 2009. MDM kinaongoza baadhi ya miji muhimu lakini hakijawahi kushinda zaidi ya asilimia 10 ya kura za kitaifa. Daviz Simango aligombea Urais mara tatu kabla kufariki 2021. Lutero Simango, 64, ni mbunge wa muda mrefu. Anadai MDM inalenga zaidi maendeleo kwa sababu hakijawahi kuwa sehemu ya jeshi, tofauti na ilivyo kwa Frelimo na Renamo.