Na
Gaure Mdee
Hii ni Ramadhan, furaha ya mwezi huu hukamilika na utamu wa futari, hata hivyo imitiwa uchungu na mfumuko wa bei barani Afrika.
Mfaume Omari, dereva wa pikipiki kutoka Sinza, Dar es Salaam hutumia muhogo kama futari yake badala ya mlo kamili, uliojaa lishe ambao umejizoelea umaarufu kipindi hiki cha Ramadhan.
"Bei imekuwa kikwazo kila sehemu," anaiambia TRT Afrika kwa unyonge. "Mafuta, Ngano, Matunda, vyote hivyo havikamatiki. Kilo moja ya nyama inagharimu shilingi 8,000(dola 3). Hali itakuwaje ikifika Eid?"
Takwimu zinaonyesha ukweli mchungu. Kutakana na utafiti wa mwaka 2021, asilimia 35 ya raia kutoka Afrika Kaskazini na sehemu za Mashariki ya Kati walifichua kuwa kupanda kwa bei kulileta changamoto kubwa zaidi huku wakizingatia ugumu wa kufunga kwa mwezi mmoja.
Shirika la Mpango wa Chakula Duniani linasema kuwa hali mbaya ya chakula iliwakumba watu milioni 349 katika nchi 79 kwa mwaka 2022. Zaidi ya watu milioni 140 walihitaji msaada, idadi ambayo haijabadilika.
Hali iko wazi kabisa
Hali hii inaashiria nini kwa familia zinazoomba unafuu katika mwezi huu wa Ramadhan wakijitayarisha na Eid?
Shabani Asmani, mkazi wa Dar es Salaam, anatabiri kuwa hali inaweza kuwa mbaya zaidi kutokana na kuendelea kwa mfumuko huo wa bei.
"Hali ya kiuchumi inaendelea kuwa mbaya zaidi kwa idadi kubwa ya watu. Bei zimepanda sana, na inaonekana kuna uwezekano ya kupanda zaidi kuelekea Eid," Asmani anaiambia TRT Afrika.
Madai haya, yanaungwa mkono na Ali Maliza, mfanyabiashara mwingine, ambaye anasema kuwa watu wanashindwa kumudu mambo ya msingi kutokana na kupanda kwa gharama za maisha .
"Hakuna anayesalimika biashara inapokwenda chini, natumai kutakuwa na unafuu wakati wa sikukuu ya Eid," anasema.
Kusini mwa jangwa la Sahara, ambapo chakula na nishati huchukua nusu ya matumizi ya kaya, kuendelea kupanda kwa gharama kumewasukuma wengi ukingoni.
Tangu janga hili, serikali zimejaribu kushusha bei ya chakula kupitia kupunguza ushuru ili kupunguza shinikizo kwa mapato ya kaya. Na hatua hizi , zimetoa unafuu wa muda.
Kadri mwezi unavyozidi kwenda mbele, ndivyo ukarimu kati ya jumuiya na vikundi vya misaada unakuwa muhimu katika kutoa mwanga wa matumaini wakati wa majaribu kama haya.
Salum Said, ambaye anaishi na familia yake katika jiji la Morogoro, Tanzania, anafichua wazi uzito wa hali hiyo. "Baada ya kula chakula cha daku, hatuli hadi muda wa futari, na chakula hicho kinapaswa kudumu hadi siku inayofuata kwa sababu, kiuchumi, hatuwezi kumudu kula mara mbili au tatu," anaiambia TRT Afrika.
Imani jasiri
Licha ya kupanda kwa gharama za chakula, mwezi wa Ramadhan unaendelea kuwaleta watu pamoja.
Mamilioni ya familia za Kiafrika pia husalia bila kutetereka kwa imani kwamba nia yao ya kufikia lengo la Ramadhan litafikiwa.
Kama anavyosema Suleiman Omari, mkazi wa Dar es Salaam, ugumu wa maisha ndio kipimo cha ibada kwa Mungu. Mwisho wa siku, ni uvumilivu na kudra zenye kushinda changamoto hizo.
"Kinachoendelea kiuchumi hakiko ndani ya uwezo wetu. Lakini Waislamu ni lazima tufunge, na Mwenyezi Mungu atatuongoza katika kipindi hiki," anasema. "Inazingatiwa kwamba bei zitapanda zaidi tunapojiandaa kwa Eid. Hata hivyo, kuvaa nguo mpya siku ya sikukuu ni sunna kwetu, na kwa namna moja au nyingine tutalishughulikia."
Hata hivyo, Salum ana matumaini kwamba baada ya wiki mbili za mwezi mtukufu, hali ya utulivu itarejea.
"Mara nyingi, bei hupanda mwanzoni na baadae kushuka. Vitu vinakuwa bei nafuu kadri tunavyosonga mbele, na wakati huu haipaswi kuwa tofauti licha ya hali iliyopo," anasema.