Lissu alirejea Tanzania Januari 2023 baada ya kifo cha Magufuli na baada ya Rais Samia Suluhu kuingia madarakani/ Picha: AFP

Mwanasiasa wa upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu amekamatwa mjini Arusha, kaskazini mwa Tanzania.

Polisi walisema walimkamata Lissu Jumapili kwa tuhuma za kufanya mkusanyiko usio halali.

"Lissu yuko chini ya ulinzi pamoja na watuhumiwa wengine watatu kwa kosa la kuitisha mikutano isiyo halali na kuzuia maafisa wa sheria kufanya kazi zao," Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo alisema katika taarifa yake.

"Washukiwa watahojiwa na hatua nyingine za kisheria zitafuata baada ya hapo," Masejo aliongeza.

Huku hayo yakiarifiwa, kiongozi wa Upinzani nchini Tanznaia, Freeman Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, amelaani kukamatwa kwa Lissu na kusema ni uonevu na unyanyasaji.

"Pia tunalaani kuzuiwa kwa mikutano yetu tuliyopanga katika maeneo ya Ngorongoro, Loliondo na Karatu," alisema Mbowe.

“Tunahofia maisha yetu. Sasa ni dhahiri kuwa serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inarudisha utawala dhalimu ambao haukuheshimu haki za binadamu, uhuru na demokrasia,” aliongeza.

Kiongozi huyo wa CHADEMA ametaka Lissu, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho na watuhumiwa wengine watatu kuachiwa bila masharti.

CHADEMA imesema watuhumiwa hao walikamatwa katika hoteli moja wilayani Karatu.

Mkosoaji wa serikali

Lissu ambaye alikuwa mkosoaji mkubwa wa aliyekuwa Rais John Pombe Magufuli (marehemu) alilazimika kukimbilia nje ya nchi baada ya kupigwa risasi 16 katika shambulio la mwaka 2017 ambalo anasema lilichochewa kisiasa.

Lissu alirejea Tanzania Januari 2023 baada ya kifo cha Magufuli na baada ya Rais Samia Suluhu kuingia madarakani.

TRT Afrika