Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Tanzania Freeman Mbowe ameachiliwa kwa dhamana, chama chake kilisema Jumamosi, baada ya kuzuiliwa siku chache kabla ya uchaguzi wa mitaa.
Uchaguzi huo unatazamwa kama kipimo cha Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye alichukua madaraka mwaka 2021 kwa ahadi za mageuzi na kuboreshwa kwa uhuru wa raia - na kuwakatisha tamaa waangalizi wa kimataifa, ambao wanaashiria kurejea kwa sera za ukandamizaji za mtangulizi wake.
Chama hicho kilisema siku ya Ijumaa kuwa yeye na watu wengine wa chama "wamezuiliwa kwa nguvu" na maafisa baada ya kutoka kwenye mkutano ambao polisi walivunja kwa kutumia vitoa machozi kusini mwa nchi hiyo.
Katika chapisho kwenye mtandao wa kijamii wa X mapema Jumamosi, Chadema ilithibitisha Mbowe na washikiliwa wengine wa chama hicho kuachiwa kwa dhamana.
'Wamepigwa sana'
“Baadhi ya wenzetu walipigwa vikali na polisi licha ya kwamba hakuna aliyepinga kukamatwa,” alisema Mbowe baada ya kuachiwa huru.
Alisema maafisa wamewashutumu kwa "kukiuka ratiba ya kampeni" na mkutano wao uliokusudiwa, wakitaja madai hayo "hayana msingi".
"Ninaamini hii ni hatua ya makusudi ya kuvuruga kampeni zetu zilizopangwa," alisema, kwenye video iliyoshirikiwa na upinzani.
Aliongeza kuwa polisi bado wanawashikilia baadhi ya wanachama wa Chadema, na kwamba yeye na wengine waliambiwa waripoti Novemba 29, lakini alikusudia kushauriana na mawakili.
Kipimo cha joto la kisiasa
Ni mwezi uliopita tu, Mbowe na naibu wake Tundu Lissu - pamoja na viongozi wengine wa upinzani - waliwekwa kizuizini kwa muda mfupi baada ya polisi wa kutuliza ghasia kuzuia mkutano mkubwa katika mji mkuu wa kibiashara wa Dar es Salaam.
Kura za maoni za mashinani zilizopangwa kufanyika Novemba 27 zinatarajiwa kuwa kipimo cha hali ya kisiasa kabla ya uchaguzi wa urais utakaofanyika Oktoba ijayo.