Katika kijiji cha Kafin-Tafawa ambacho ni moja wapo ya vijiji visivyoelezeka ambavyo vipo kaskazini mwa Nigeria katika jimbo la Bauchi – Duka dogo lililo nakshiwa kwa rangi ya njano limetingwa na shughli za kiuchumi.
Watu wanapanga foleni kwa ajili ya miamala ya kifedha, Hassan Abdullahi anachukua nafasi kama mhudumu wa benki – hana kingine isipokuwa mashine ya kutelezesha kadi kuweka fedha, yaani kituo cha mauzo-POS kwa lugha za kibenki.
Abdullahi anawasaidia watu kufanya uhamisho wa fedha, kutoa fedha au kufanya malipo kwa kutumia kifaa kidogo. Kwa wateja wanaotoa pesa, anawapa fedha taslimu mara baada ya kutumia kadi zao za kuweka fedha kwa kuhamishia kiwango husika katika akaunti yake.
Kwa wale ambao wanataka kutoa pesa au kufanya malipo, anachukua pesa halafu anazihamishia kwenye akaunti za benki ambazo wateja wanataka zielekezwe. Anachaji kiwango fulani kwa kila muamala.
Wanafahamika kama ‘opareta wa POS’, maelfu ya watu kama Abdullahi wanahudumu kuleta mabadiliko nchini Nigeria, ambako taasisi za kibenki zimepenya kwa uchache kabisa.
Mpango ulioanzishwa na Benki Kuu ya Nigeria haujasaidia kupeleka huduma za kibenki vijijini pekee lakini pia kutoa wigo wa ajira kwa wengi kwenye nchi yenye zaidi ya watu milioni 200.
Hata hivyo, maopareta wa POS si waajiriwa wa benki lakinii ni mawakala ambao wanabadilisha uchumi mkubwa wa Afrika.
Biashara inayoshamiri
Kijiji cha Abdullahi hakina benki hata moja, au japo hata mashine ya ATM. Kwa watu kufanya miamala ya kifedha kama maeneo mengine mengi ya vijijini nchini Nigeria.
Kwa hiyo, alipofungua duka mwaka 2021 alifungua fursa nyingine pia kwa wanakajijiji.
Kijana huyo mwenye umri wa miaka 30 ambaye hakufanikiwa kuhitimu masomo yake anaiambia TRT World kwamba alianzisha biashara yake kutokana na mkopo mdogo alioupata toka kwa dada yake. Sasa anaingiza kipato cha kati ya Naira 50,000 ($112) na 60,000 ($135) kwa mwezi, mara mbili ya kima cha chini cha mshahara nchini Nigeria.
“Pesa hii inanisaidia kutunza familia yangu” na wakati mwingine “kusaidia wengine,” anaeleza.
Abdullahi anasema anafurahia mafanikio yake na anatarajia kujiunga na chuo kikuu kwa masomo ya shahada ya kwanza ambayo hakuweza kujiunga nayo baada ya kuhitimu elimu ya sekondari miaka kadhaa iliyopita sababu ya changamoto za kiuchumi.
“Naamini kwamba naisaidia jamii yangu pia, kwa sababu bila vituo vya mauzo watu walikuwa wamekwama na kuchanganyikiwa” anaongeza.
Abdullahi ni mmoja ya watu wanaokadiriwa kufikia milioni 1.4 wengi wao wakiwa ni vijana ambao wamejiajiri moja kwa moja kwenye vituo vya mauzo katika nchi ambayo umasikini na tatizo la ukosefu wa ajira vipo juu sana.
Hivi vituo vya mauzo vinafanyika kwa kiasi kikubwa na biashara ndogondogo, watu wenye kipato cha chini, na jamii ya watu wasio katika huduma za kibenki, mijini na vijijini. Lakini ukubwa na upana wa miamala ni mikubwa na inazidi kuongezeka.
Takwimu kutoka benki kuu ya Nigeria zinaonesha kwamba, miamala ya kifedha yenye thamani ya Naira trilioni 6.4 (USD 14.2 bilioni) ilifanyika kwa kupitia vituo vya mauzo kwa mwaka 2021, ikiwakilisha ongezeko la asilimia 36 kutoka mwaka uliopita. Kiwango cha miamala ya kifedha ilikuwa ni takribani asilimia 47 ya bajeti kuu ya Nigeria kwa mwaka 2021.
Kwa mwaka 2022 kiwango kitapanda zaidi kwani tayari kimeshavuka Naira trilioni 6 mpaka mwezi septemba.
Msukumo wa kidigitali
Mwaka 2012, Benki kuu ilikuja na “sera ya mauzo bila noti” ili kudhibiti idadi ya pesa katika mzunguko na kutia moyo matumizi ya benki za kidigitali. Hii kwa kiasi kikubwa imesaidia kuinua biashara ya POS.
Benki ya Apex pia inautambua mchango wa vituo vya POS kwa kuwaleta wanigeria wengi zaidi katika mfumo wa kibenki, hasa kwa wale wa maeneo ya vijijini.
Kwa mujibu wa Isa Abdullahi, mhadhiri mkuu wa Kitengo cha Uchumi na Maendeleo wa Chuo Kikuu cha Shirikisho katika mji wa Kashere, uanzishwaji wa biashara ya POS ilikuwa ni “Moja ya vitu bora kabisa kuwahi kutokea katika uchumi” kwa miaka ya hivi karibuni .
Anasema ilikuwa na msingi kwa sababu “ya uwezo wake wa kuajiri watu,” hasa wale ambao hawakuweza kuendelea na shule na kufanya miamala ya kipesa “kuwa rahisi zaidi.” Katika kuongezea, anasema umaarufu wake umeongezeka zaidi na kukubalika kwa sababu mawakala wa pesa “wapo mlangoni kwako”
Mtazamo huu pia anao Victor Ojolo, rais wa Shirikisho la PesaSimu na Mawakala wa benki, ambao wanawakilisha wafanyabiashara wa POS nchini Nigeria.
Anaiambia TRT World kwamba mchango wao katika uchumi ni “wa kipekee”. Anasema biashara ya POS imetengeneza ajira nyingi sio tu kwa mawakala wa fedha bali pia biashara nyingine tanzu, kama vile wale wanaotengeneza karatasi kwa ajili ya risiti za miamala kama sehemu ya “mnyororo wa thamani”. Hii ni muhimu katika kushughulikia ukosefu wa ajira nchini Nigeria, ambayo ilifikia asilimia 33 kwa mwaka 2021.
“Biashara ya POS imeleta mapinduzi ya kibenki nchini Nigeria,” anasema, akiongeza kwamba zinapatikana hata katika maeneo ambayo “benki bado hazijafikiria.”
Changamoto zilizopo
Mbali na kuongeza kasi na kuongezeka umaarufu kwa biashara ya POS, bado inakumbwa na changamoto kadhaa ambazo zinaikumba sekta ya mawakala wa benki binafsi na wateja wao. Kwa mfano, asilimia kubwa ya wateja wanalalamika kuhusu pesa kutowekwa kwenye akaunti wanazodhamiria baada ya kutolewa toka kwa mtumaji.
Wataalamu wanaelezea tatizo hili kwamba linatokana na kufeli kwa seva za benki, Kuvunjika kwa mawasiliano ya ndani au changamoto za kimtandao kwenye vituo vya POS. Wateja na waendeshaji wa POS wamekuwa wakilalamika mara kwa mara kwamba imekuwa ikichukua muda mrefu wakati mwingine hata wiki nzima kurekebisha makosa ya muamala au kurudisha muamala, kitu ambacho kinawaweka wateja katika wakati mgumu kifedha hasa kwa watu wa kipato cha chini.
Victor Olojo anasema changamoto nyingine ni mawakala wa serikali katika baadhi ya majimbo wanakusanya “Kodi zaidi ya moja” toka kwao kitu ambacho kinaathiri biashara zao “ndogondogo”. Anaomba uwepo mfumo wa uwazi katika mpango kazi mzima wa taasisi katika utendaji kazi na mchakato wa ukusanyaji kodi. Anaendelea kusema kwamba ushirika pamoja na mamlaka zimekuwa zikifanya kazi pamoja katika kutatua changamoto hizo.
Wakati sekta ya fedha nchini Nigeria ikiwa inapitia mabadiliko makubwa na benki kuu ikizidi kuongeza juhudi za kuhakikisha uchumi unaenda “bila utumiaji wa noti”, Ojolo anaamini kwamba POS na huduma nyingine za kipesa “kwa hakika ndio mfumo ujao katika miamala kwa njia ya simu” katika taifa.
‘POS ni mkombozi’
Tukirudi kwenye duka la POS la Abdullahi pale Kafin Tafawa, ni biashara kama kawaida ambapo Hassan Hamidu anatoa fedha kwa ajili ya kununua chakula cha familia yake ya watu 15 “Mimi ni mteja wa kila siku wa POS,” anasema, huku akitanabaisha POS kama “mkombozi”.
Mtumishi wa Umma mwenye umri wa miaka 50 anakumbuka jioni moja ambapo huduma ya POS ilimsaidia kupata pesa za kumkimbiza mtoto wake hospitali. “Ilikuwa ni dharura lakini sikuwa na pesa,” anaelezea. Hata hivyo aliweza kwenda kwenye duka la POS mtaani kwake, kutoa pesa ndani ya dakika chache na kumkimbiza mwanae hospitali.
Anaeleza kwamba, kama angeenda benki mjini au kwenye ATM kupata fedha, ingemchukua angalau saa moja na nusu jambo ambalo “lingeweza kuhatarisha maisha ya mwanae.”
Hamidu hayuko peke yake
Mamilioni ya Wanigeria pamoja na biashara ndogondogo katika maeneo ya vijijini pamoja na maeneo ya miji mikubwa kama vile mji mkuu, Abuja, na mji wa kibiashara wa Lagos na Kano zinategemea kwa kiasi kikubwa maduka ya POS kwa miamala ya kifedha sababu ya upatikanaji wake muda wote na urahisi wa kuutumia.