Kamishna wa masuala ya Wakimbizi Kenya, John Burugu ametoa amri kwa wakimbizi wote wanaopewa hifadhi nchini humo, kuwasilisha pasi zote walizonazo kutoka nchi zai asili la sivyo wachukuliwe hatua.
Kamishna Burugu alisema kuwa ametoa muda wa siku thelathini kwa wakimbizi wote ambao bado wanashikilia pasipoti zao kuziwasilisha kwa idara ya huduma ya Wakimbizi ambapo badala yake watakapokea stakabadhi halali za wakimbizi kwa mujibu wa sheria za kimataifa.
''Wakimbizi wana haki ya kupewa hati za Kiraia, utambulisho, na kusafiri, zikiwemo Hati za kusafiri maalum zinazosomeka (CTDs) kwa ajili ya kusafiri nje ya Kenya, isipokuwa katika nchi yao ya asili,'' alisema Burugu katik ataarifa.
Hatua hii imekuja kufuatia wasiwasi kuwa baadhi ya wakimbizi wamekuwa wakitumia pasi hizi kusafiri nje ya nchi, kinyume na sheria za kimataifa na za wakimbizi wa ndani.
Katika taarifa iliyochapishwa katika mtandao wa X, zamani twitter, Burugu alisema wale watakaokutwa kutumia pasipoti hizo watakabiliwa na sheria.
“Kushindwa kutii agizo hili kunaweza kusababisha madhara ya kisheria kama ilivyoainishwa katika mkataba wa kimataifa uliotajwa hapo juu na Sheria ya Wakimbizi Na. Kifungu cha 17 cha Sheria ya Wakimbizi,” alionya Burugu.
Kenya inawahifadhi wakimbizi kutoka nchi jirani zinazokumbw ana mizozo, ikiwa na takriban wakimbizi 623,500 waliosajiliwa na wanaotafuta hifadhi . Asilimia 86 ya wakimbizi hao wanatoka Somalia na Sudan Kusini.