Rais wa Kenya William Ruto ameongoza sherehe ya kufuzu kwa makurutu wapya wa jeshi, katika Chuo cha Majeshi kinachoitwa Defence Forces Recruits Training school, mjini Eldoret.
Sherehe hiyo ilianza kwa rais kuwaomba watu kusimama kwa dakika moja ya ukimya kama ishara ya kuwaheshimu maafisa wa jeshi waliopoteza maisha katika ajali ya ndege mwezi Aprili ambayo pia alikuwepo Mkuu wa Majeshi Jenerali Francis Ogolla.
"Sherehe hii inaashiria hitimisho la msingi wa mafunzo ya kijeshi kwa vijana wazuri na wenye ujasiri na wanawake kabla yetu, wakikaribisha mwanzo wa kazi katika vikosi vyetu vya ulinzi ambayo hakika itakuwa changamoto ambayo italeta matukio mema," Rais William Ruto amesema wakati akihutubia katika sherehe hiyo.
Jeshi la Kenya linasema mafunzo waliyoyapitia yalikuwa na nia ya kuwabadilisha kutoka raia hadi kuwa askari hodari. Wakati wa mafunzo ya kijeshi walipimwa katika ngazi na viwango tofauti kwa kuzingatia miongozo ya ulinzi ya Kenya.
"Mafunzo yenu yamewapa ujuzi wa kimsingi ili kusaidia kukuza tabia, nidhamu, na ujasiri wa kufanikiwa kuanza kazi ya jeshi," Rais aliongezea.
"Kikundi hiki kinasimama kwa ukubwa wake wote na tofauti, ikiwa idadi ya wanawake wanaohitimu pamoja na wenzao wa kiume wameweka rekodi mpya. Hii inaashiria kujitolea kwa jeshi la KDF na serikali kwa usawa wa kijinsia," Rais Ruto ameongezea.
Maafisa hawa wapya wa kijeshi watahudumu katika vitengo tofauti za usalama wa jeshi ardhini na majini.