Zawadi kubwa ya fedha itatolewa kwa mtu yeyote wa umma atakayetoa taarifa za kuaminika zitakazosaidia kukamatwa kwa mtuhumiwa yeyote. Picha: Wizara ya Mambo ya ndani Kenya

Serikali ya Kenya kupitia Wizara yake ya Mambo ya ndani hii leo imetoa orodha ya majina ya washukiwa wa ugaidi na kuongeza kuwa ni tangazo la vita dhidi ya magaidi wenye silaha hatari na kuwa wanachama wa kundi la Al Shabaab.

Serikali hiyo imesema kuwa, majina iliyotoa ni ya watu waliohusika kwenye visa mbalimbali ya mauaji ya kikatili ya hivi karibuni dhidi ya raia wake na maafisa wake wa usalama katika eneo la Lamu na viunga vyake ikiwemo msitu wa Boni.

"Mashambulizi kadhaa ya Al shabaab yamefanyika, na kusababisha mauaji ya kikatili ya raia wasio na hatia na wafanyikazi wa usalama ndani ya kaunti ya Lamu na Eneo la Boni kwa ujumla." alisema waziri Kindiki.

Wizara hiyo ya usalama wa ndani inasema kuwa magaidi hao wafikao 35 wanaotafutwa, wanahusika kwenye utegaji wa vilipuzi (IEDs) kwenye barabara mbalimbali eneo la Lamu na shambulio la kambi ya kijeshi ya Marekani ya Manda Bay mnamo tarehe 5 Januari 2020.

Aidha, Serikali ya Kenya imewataka washukiwa hao ambao majina na picha zao zilisambazwa katika vyombo vya habari kujisalimisha kwa vituo vya Polisi nchini humo.

"Washukiwa wanaamriwa kujisalimisha kwa kituo chochote cha Polisi nchini Kenya mara moja. Zawadi kubwa ya fedha itatolewa kwa mtu yeyote wa umma atakayetoa taarifa za kuaminika zitakazosaidia kukamatwa kwa mtuhumiwa yeyote", Wizara ilisema.

TRT Afrika