Paul Mackenzie anashitakiwa kwa kuwashawishi watu wasile ili 'wamuone Yesu'  / Picha: Reuters

Mamlaka nchini Kenya imepiga marufuku makanisa matano likiwemo lile la mshukiwa wa kiongozi wa dhehebu ambapo wafuasi 400 walikufa wakiamini ibada ya njaa.

Msajili wa vyama alisema katika tangazo ya Gazeti la Kenya kwamba leseni ya mtu anayejiita mchungaji Paul Nthenge Mackenzie Good News International Ministries imepigwa marufuku kuanzia tarehe 19 Mei.

Mackenzie anadaiwa kuwachochea wafuasi wake kufa njaa ili “kukutana na Yesu” katika kisa ambacho kimewashangaza sana Wakenya.

Wakati njaa inaonekana kuwa sababu kuu ya vifo, baadhi ya waliyo adhirika - ikiwa ni pamoja na watoto - walinyongwa, kupigwa au kuzidiwa, kulingana na uchunguzi rasmi wa maiti.

Uchunguzi

Mamlaka pia ilipiga marufuku makanisa mengine manne ikiwa ni pamoja na 'New Life Prayer Centre' na Kanisa linaloongozwa na mwinjilisti mahiri Ezekiel Odero, ambaye amekuwa anahusishwa na Mackenzie.

Odero anachunguzwa kuhusu mashtaka mengi yakiwemo mauaji, kusaidia kujitoa mhanga, itikadi kali na utakatishaji fedha.

Kukamatwa kwake mwezi Aprili kulifuatia kupatikana kwa miili ya watu katika msitu wa Shakahola karibu na mji wa pwani wa Malindi, huku polisi wakisema miili hiyo ni ya wafuasi wa Mackenzie.

Huku waendesha mashtaka wakiwahusisha wahubiri hao wawili, Odero aliachiliwa kwa dhamana mwezi Mei huku mahakama wiki jana iliongeza kizuizi cha Mackenzie kwa siku 47 zaidi kusubiri uchunguzi zaidi.

Msajili wa vyama pia alifutilia mbali usajili wa kanisa la 'Helikopta of Christ' ya askofu Thomas Wahome, kanisa la 'Theophilus' na Kanisa la 'Kings Outreach'.

Kifungu cha 12 (1) cha Sheria ya vyama nchini Kenya kinampa msajili mamlaka ya kufuta leseni ya jumuiya ikiwa kuna uwezekano wa kufuata au kutumika kwa madhumuni yoyote kinyume cha sheria.

Kuna zaidi ya makanisa 4,000 yaliyosajiliwa Kenya kulingana na takwimu za serikali.

TRT Afrika