Rais wa Kenya William Ruto, amependekeza kupunguzwa kwa idadi ya viti vya wabunge katika Bunge la Afrika, yaani Pan Africa Parliament (PAP) kutoka 275 hadi 110.
Amesema hii itapunguza gharama ya uendeshaji wa bunge hilo.
Bunge la Afrika ni jukwaa linalowakilisha mataifa yote ya Afrika katika mijadala na kufanya maamuzi kuhusu matatizo na changamoto zinazokabili bara hili. Bunge liko Midrand, Afrika Kusini.
"Leo hii, bajeti ya Umoja wa Afrika inaidhinishwa na watu ambao si wawakilishi wa watu. Tunataka watu wa Afrika wachukue jukumu la bara hili,” alisema.
Amesema itakuwa bora ikiwa kila nchi itawakilishwa na mwanamme na mwanamke mmoja.
Kwa sasa kila nchi inawakilishwa na wajumbe watano katika bunge hilo.
Pendekezo lake ni mojawapo ya mapendekezo ya kufanya mabadiliko katika operesheni ya Tume ya Umoja wa Afrika.
Bunge la Afrika?
Marais na viongozi wa Afrika waliamua kuundwa kwa bunge la Afrika katika mkutano wao wa Juni 2014.
Badala ya kuchaguliwa moja kwa moja na wananchi, wanachama wa PAP huteuliwa na mabunge ya nchi zao na wajumbe wa mabunge yao ya ndani.
Bunge linaundwa na wajumbe watano kwa kila nchi ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa angalau muakilishi mwanamke kutoka kila nchi.
Lengo kuu kulifanya Bunge hilo kuwa taasisi yenye mamlaka kamili ya kutunga sheria, ambayo wajumbe wake wanachaguliwa kwa kura ya maoni ya wote. Hadi wakati huo, PAP ina mamlaka ya ushauri, na usimamizi wa bajeti ndani ya AU.
Bunge linaweza kupendekeza rasimu ya sheria za kielelezo na kutoa mapendekezo yake yenyewe kuhusu masuala au maeneo ambayo linaweza kuwasilisha, au kupendekeza rasimu ya sheria kwa Bunge kwa ajili ya kuzingatiwa na kuidhinishwa na viongozi wa Afrika.
PAP inapaswa kukutana angalau mara mbili katika kikao cha kawaida ndani ya kipindi cha mwaka mmoja. Vikao vya Bunge vinaweza kudumu hadi mwezi mmoja.
PAP pia inaweza kukutana katika vikao vyengine ikiwa kuna sababu muhimu.
Kamati za bunge hili ambazo ni kumi zinawakilisha sekta tofauti barani hukutana mara mbili kwa mwaka (Machi na Agosti) katika mikutano ya kisheria na zinaweza kukutana mara nyingi zaidi wakati wa vikao vya bunge au katika mikutano isiyo ya kisheria pindi inapohitajika.
Mabadiliko kwa Tume ya AU
Kenya iliteuliwa na mkutano wa marais Februari 2024 kuwa Bingwa wa Umoja wa Afrika katika Mageuzi ya Kitaasisi.
Rais William Ruto amechukua jukumu hili kutoka kwa Rais Paul Kagame wa Rwanda.
Anatarajiwa kukamilisha mpango kamili wa marekebisho ya Kitaasisi ulioanza mwaka wa 2016.
Marekebisho hayo yanahusisha muundo, utendaji kazi na mwelekeo wa Tume ya Umoja wa Afrika, Mashirika ya AU na Mashirika Maalumu ili yawe na ufanisi zaidi katika kusimamia mipango ya Umoja wa Afrika.
FDB