Wateka nyara wataka kulipwa $12,000, wakidai ni pesa walizolipa kuwanunua mateka. /Picha : AP

Serikali ya Kenya imetoa onyo kwa raia wake kutosafiri Myanmar huku kesi za uteka nyara na utumwa kuzidi.

Nchi hiyo imekua ikikabiliwa na migogoro ya ndani na hivyo kusababisha kuenea kwa uhalifu.

Balozi wa Kenya nchini Thailand, Kipitness Lindsay Kimwole amewaonya raia wa Kenya kutotafuta kazi Myanmar kwa njia ya mitandao akisema mitandao hiyo inatumiwa na wahalifu kuwalaghai.

Ubalozi umeelezea wasiwasi wake kuendelea kwa raia wa Kenya kutuma maombi ya kazi nchini humo licha ya kuwa kuna hatari kubwa ya kutekwa nyara, utumwa na kuadhibiwa na wahalifu.

‘’Ubalozi wa Kenya nchini Thailand kwa mara nyingine yatoa onyo kwa raia wa Kenya kutosafiri kwenda Myanmar. Onyo hili latolea huku kukiwa na dazeni ya Wakenya wakiomba kunusuriwa kutokana na magenge wahalifu na mazingira magumu, huku wengine bado wakimiminika nchini humo na kuwa wahanga wa magenge wahalifu kutoka China, wanaofanya biashara ya uteka nyara na utumwa’’.

Balozi Amb Kimwole amesema katika taarifa iliyotolewa na vyombo vya habari nchini Kenya.

Kulingana na balozi huyo hadi sasa kuna Wakenya 10 waliokamatwa na genge hilo, ambalo linadai kulipwa fidia kwa mamilioni ya pesa ili kuwaachilia huru.

Aidha balozi amesema kuwaokoa Wakenya hao kutoka mikononi mwa wahalifu imekua ni biashara, kwa sababu wanadai kurudishiwa dola 12,000 za Marekani, ambazo ni pesa walizotumia kuwanunua kama watumwa.

Kulingana na Wizara ya Mambo ya Nje na Masuala ya Diaspora ya Kenya, Wakenya wamekwenda huko kinyume na maagizo ya Serikali ya kutosafiri kuelekea nchi hiyo, na hivyo kulazimika kulipa fidia, ili kuachiliwa huru.

Vile vile wizara hiyo imesema, shida hiyo imezidi kuwa kubwa baada ya Wakenya wengine kuwashawishi wenzao wajiunge pamoja nao kwa kuwapatia ahadi za ajira za uwongo na baadae kuwateka nyara.

Wizara hiyo pia imesema imekuwa ikishirikiana na mamlaka za nchi ya Thailand kuwaokoa watu kutoka 141 kutoka nchi za Afrika, Wakenya 108 , Waganda 19, Waethiopia 11, Mburundi mmoja, Mzimbabwe na Msenegali.

TRT Afrika