Kenya yaongeza usalama Lamu baada ya mashambulizi

Kenya yaongeza usalama Lamu baada ya mashambulizi

Serikali inasema mashambulizi yalifanywa Jumatatu na takriban watu 60
Mji wa Lamu umepata mashambulizi ya kigaidi mara kwa mara tangu takriban mwaka 2014 / Picha: Reuters

Serikali ya Kenya imeongeza usalama katika mji wa Lamu, pwani mwa nchi kufuatia mashambulizi ya kigaidi siku ya Jumatatu.

"Opereshensi inayoendeshwa na maafisa wa polisi na wanajeshi unaedelea," ripoti kutoka kwa waziri wa mambo ya ndani Kithure Kindiki imesema.

Watu wanaoshukiwa kuwa magaidi waliwavamia wasafiri katika barabara kuu ya Lamu witu Garsen. Mtu mmoja aliuawa na wengine 10 kujeruhiwa.

"Maafisa wa usalama kutoka Nyangoro waliokuwa wameshika doria kwenye barabara kuu walijibu haraka na kuwavamia magaidi takriban 60 na kuwatawanya katika msitu wa Boni," Kindiki ameongezea,

Mashambulizi Lamu

Mashambulizi katika eneo hili la pwani Kenya na magaidi wa Al shabaab yamefanyika mara kwa mara tangu takriban mwaka 2014.

Lamu inapakana na Somalia na hii huwarahisishia magaidi kusafirisha silaha haramu zinazoweza kutumika kwa uhalifu huo.

Msitu wa Boni ambao unapakana na Somalia pia unaifanya iwe rahisi kwa uvamizi wa Al-Shabaab. Msitu huu imeripotiwa kuwapa nafasi magaidi sehemu ya kufanyia mafunzo na pa kukimbilia baada ya kufanya mashambulizi.

Baada ya jeshi la Kenya kuingia Somalia mwaka wa 2011 kwa ajili ya kusaidia Somalia kupambana na magaidi wa al-Shabaab, kundi hilo lilitaka Kenya kujiondoa Somalia .

Jeshi la Kenya lilifaulu kuwafukuza kundi hilo la kigaidi kutoka bandari ya Kismayu kusini mwa Somalia na miji mingine muhimu, na baada ya hapo vikosi vya Kenya vikajiunga na vikosi vya Umoja wa Afrika (AU) vyaa kusaidia amani nchini Somalia.

TRT Afrika