Kenya yaondoa vikwazo vya Uviko19 kwa wasafiri  / Photo: Reuters Archive

Unapoingia Kenya sasa hauhitaji tena kuthibitisha kuwa hauna virusi vya Uviko19.

Waziri wa Afya inasema wasafiri sasa wanaweza kuingia nchini bila ukaguzi wowote unaohusiana na Uviko 19.

"Wasafiri wote wanaowasili nchini kupitia bandari yoyote ya kuingia hawata hitajika tena kuonyesha uthibitisho wa chanjo cha Uviko 19 au vipimo vya kabla ya kuondoka (nchini) vya Uviko 19," ilisema taarifa ya Waziri wa Afya, Nakhumicha Wafula.

Madereva wa malori wanaoingia nchini pia hawalazimishwi tena kuwa na uthibitisho wa kutokuwa na maambukizi ya Uviko19.

"Wasafiri ambao watawasili katika bandari yoyote ya kuingia nchini wakiwa na dalili kama za mafua watatarajiwa kujaza fomu za kuonyesha usafiri wao." anaongeza.

Pia watahitajika kuchukua kipimo cha Uviko19, cha papo hapo kwa gharama zao wenyewe, watakapowasili.

"Mtu anayesafiri nje ya nchi atalazimika kuzingatia mahitaji ya kiafya yanayohusiana na Uviko19 ya nchi anakoenda," Waziri alisema.

Uamuzi wa Kenya unakuja siku chache baada ya Shirika la Afya Ulimwenguni, World Health Organisation, kutangaza kwamba Uviko 19 sio dharura ya kiafya tena, na sio wasiwasi wa kieneo na kimataifa.

TRT Afrika