Mshukiwa mkuu wa sakata ya zadii ya dola milioni moja amekamatwa nchini Kenya.
Kitengo cha makosa ya jinai DCI, kinaelezea kuwa kontena mbili zilizojazwa mchanga zilizotangazwa kama madini ya Tantalum zilikutwa katika bandari ya Mombasa, pwani mwa Kenya.
Tantalum, kama poda ya chuma hutumika katika utengenezaji wa vifaa vya umeme.
Mshukiwa ametiwa mbaroni na Kitengo cha Usaidizi wa Operesheni (OSU) cha DCI wakati huo.
Kitengo cha DCI Kenya kimeeleza katika akaunti yao ya X kuwa Ulundu Patrick Lumumba anayejiita pia Gabriel Kulonda na wakati mwingine Lumumba Patrick Byarufu alikamatwa katika mtaa wa Harambee Avenue jijini Nairobi.
Hii ilikuwa dakika chache baada ya kuwatoroka maafisa wa uhamiaji wa uwanja wa ndege wa kimataifa ya Jomo Kenyatta, JKIA. Huku kukiwa na amri ya kumsimamisha iliyokuwa imewekewa pasipoti yake .
"Alitumia kitambulisho cha Uganda kuingia nchini ya nambari 020841009 kwa majina ya Lumumba Patrick Byarufu, na alipokamatwa pia alipatikana akiwa na Pasipoti nyingine ya Congo nambari OPO792312 kwa majina ya Patrick Ulundu Lumumba," kitengo cha DCI kimesema.
Katika kesi hiyo anayohusishwa nayo, mwanamke mmoja raia wa China alipoteza dola za Marekani 1,159,309 ( Shilingi za Kenya 151 milioni) kutokana na njama za mtuhumiwa huyo baada ya kontena moja kati ya tatu yaliyotangazwa kuwa na madini ya tantalum kupatikana ikiwa imebeba mchanga, na kusababisha uchunguzi katika bandari ya Mombasa mahali mali hiyo ilikuwa inapita.
"Cha kushangaza, kontena la futi 40 lilikuwa limepitisha michakato yote ya uthibitishaji bila hati yoyote. Mkontena 6 ya mchanga yalitangazwa kuwa madini ya tantalum," DCI iliongeza katika taarifa.
Makontena mengine mawili yalikuwa yameondolewa na kusafirishwa hadi Dubai, na juhudi zinaendelea ili kuzizuia.
DCI imesema kuwa Baadhi ya maafisa wa bandari wanaoaminika kuhatarisha ukaguzi wa usalama ili kuwezesha shughuli hizo haramu pia wanachunguzwa.