Makamu wa rais ya Kenya, Rigathi Gachagua amesema ataandaa kikao kwa ajili ya kujadili jinsi ya kukabiliana na mvua za El Nino.
"Wiki ijayo nitaitisha Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Dharura, pamoja na mashirika yote ya serikali, washirika wa maendeleo, Shirika la Msalaba Mwekundu, mashirika ya kimataifa na wadau wengine wote ili kujadili maandalizi ya mvua za El Nino zinazotarajiwa,” amesema Naibu Rais.
Utabiri wa hali ya hewa unaonyesha kuwa kati ya mwezi Oktoba hadi Disemba 2023 kuna uwezekano mkubwa wa hali ya mvua nyingi kuliko kawaida katika sehemu nyingi za Pembe za Afrika.
Idara ya Hali ya Hewa ya Kenya mwezi Agosti ilitoa onyo la utabiri wa hali ya hewa kwamba mvua kubwa inatarajiwa kunyesha mwaka huu nchini, kuanzia Oktoba hadi Januari 2024.
Kituo cha Utabiri wa Hali ya Hewa cha IGAD kinasema kwamba, mvua hiyo itaathiri maeneo ya kusini mwa Ethiopia, mashariki mwa Kenya, na kusini mwa Somalia.
Oktoba hadi Disemba ni msimu muhimu wa mvua, hasa katika maeneo ya Ikweta ya Pembe Kubwa ya Afrika, na kuchangia asilimia 20 hadi 70 ya jumla ya mvua kwa mwaka.
El Nino ni nini?
"El Niño ni hali ya ongezeko la joto katika bahari ya Pasifiki ya kati na mashariki, " mtaalamu wa utabiri wa hali ya hewa katika kituo cha ICPAC, Hussen Seid, amefafanua.
" Kuwepo kwa El Niño kunaathiri mwelekeo wa hali ya hewa kote ulimwenguni. Tukio jengine la msingi lijulikanalo kama ‘Indian Ocean Dipole’ linaendelea kukuwa katika bahari ya Hindi na kutarajiwa kuzidisha athari na matokeo ya El Niño,” Seid ameongezea.
Mara ya mwisho Kenya kukumbwa na hali ya El Nino ilikuwa mwaka wa 2006, na msimu mbaya zaidi wa El Nino ulitokea 1997.
Shirika la Hali ya Hewa Ulimwenguni linasema El Nino hutokea kwa wastani kila baada ya miaka miwili hadi saba, na vipindi vya kawaida vya mvua hii vyingi huchukua miezi tisa hadi 12.
Kutokana na wingi wa mvua hizo, mara nyingi El Nino huambatana na uwezekano wa kuwepo kwa mafuriko na maporomoko ya ardhi pamoja na mlipuko wa magonjwa kama vile malaria na homa ya dengue.
Shirika la Afya Duniani limetaka watu kujitayarisha kwa uwezekano wa kuwepo kwa maradhi kama malaria na homa ya dengue na chikungunya.
Uzalishaji wa chakula huenda ikaathiriwa vilevile, kwani mvua nyingi itaharibu chakula mashambani na kusababisha uhaba wa chakula cha kutosha sokoni hivyo kuongezeka kwa bei ya chakula.