Maandamano nchini Kenya yameingia wiki ya tatu/ picha:  Reuters

Serikali ya Kenya imeziandikia balozi na wawakilishi wa nchi tofauti waliopo nchini Kenya ikisisitiza kuwa Kenya bado iko salama. Hii inakuja baada ya nchi kuingia katika wiki ya tatu ya maandamano ambayo yameonyesha kupinga uongozi wa rais William Ruto.

"Ningependa kuwahakikishia usalama wa kudumu hautahatarishwi na hivyo basi serikali imechukua hatua kuzuia maandamano ambayo yanaleta ghasia na kuzidisha ulinzi unaoruhusiwa kikatiba," imesema taarifa kutoka Katibu Mkuu wa Baraza la Mawaziri na Waziri wa Mambo ya Nje, Musalia Mudavadi.

"Serikali itaendelea kulinda taasisi za umma na kuhakikisha usalama wa mali ndani ya nchi," taarifa imeongezea.

Kwa wiki ya tatu sasa Kenya imeshuhudia maandamano ambayo hayajawahi kutokea yakichochewa na mjadala wa kitaifa kuhusu mswada wa fedha wa 2024.

Yameongozwa hasa na vijana maarufu, Gen Z.

"Kilichoanza wakati maandamano makali yaligeuka kuwa ya vurugu na kusababisha hasara ya maisha na uharibifu wa mali ya umma na ya watu binafsi," amesema Mudavadi.

Waandamani wengine walibeba majeneza kma ishara ya kupinga mauaji ya waandamanaji / Picha: Reuters 

"Vyombo vya habari vinaendelea kukabiliana na mlipuko mkubwa wa taarifa potofu na upotoshaji katika mitandao ya dijitali. Tunakubali wasiwasi halali ulioibuliwa na vijana wetu wengi wa Kenya haswa juu ya ukosefu wa ajira kwa gharama ya juu ya maisha ambayo husababishwa na kupuuzwa kisiasa na fursa finyu za kutumia ubunifu wao na uwezo wao wa nguvu," ameongezea.

Kwa wiki mbili za kwanza maandamano yalikuwa ya amani huku vijana wakiingia mitaani na kupaza sauti zao dhidhi ya masuala kadhaa ambayo hawakubaliani nayo katika serikali ya Rais William Ruto. Hata hivyo, mambo yalionekana kubadilika baada ya vijana kuvamia bunge na kuchoma maeneo yake.

Maandamano ya Julai 2, 2024, yameonyesha uharibifu mkubwa wa mali ya watu hasa jijini Nairobi, huku waandamanaji wakifanya uvamizi na wizi.

Serikali imesema inawasaka wahalifu waliofanya vurugu katika maandamano ya Jumanne / Picha: AFP

Kitengo cha upelelezi cha nchi kimesema kinawasaka waliohusika katika vurugu na imeomba wananchi kutoa video au picha yoyote ambayo inaweza kusaidia kuwatambua.

"Waandalizi wa ghasia za leo ( Jumanne) katika maeneo ya Nairobi, Mombasa na maeneo mengine ya nchi wanaripotiwa kupanga kurudia machafuko na uporaji wao wa kikatili tena Alhamisi na Jumapili wiki hii na pengine mara nyingi zaidi katika siku zijazo," Kithure kindiki, Waziri wa Mambo ya ndani alisema pia katika taarifa akitoa uhakikisho kuwa wahalifu watasakwa.

Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya Kenya imesema watu 39 waliuawa wakiwa katika maandamano.

TRT Afrika