Baadhi ya majaji wa EACJ wakiendelea na vikao vyao ndani ya Mahakama hiyo iliyopo Arusha, Tanzania./Picha: Wengine

Mwanasheria Mkuu wa Kenya Justin Muturi ameiomba Mahakama kuu ya nchi hiyo kuzingatia upya athari za maamuzi ya kisheria yanayotolewa na Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ).

Kulingana na Muturi, idadi kubwa ya maamuzi yatolewayo na Mahakama hiyo inayopatikana Arusha, Tanzania hukinzana na yale ya Mahakama ya Juu ya Kenya.

Muturi alitoa mfano wa maamuzi ya EACJ kwenye shauri la Martha Karua dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Kenya, ambapo Mahakama hiyo iliamuru mwanasiasa huyo kulipwa Dola za Kimarekani 25,000, huku ikidai kuwa Mahakama ya juu ya nchi hiyo ilikiuka haki ya kusikilizwa kwa mwanasiasa huyo.

Mwaka 2019, Mahakama hiyo ilisisitiza kuwa baadhi ya vipengele kwenye Sheria ya Muswada wa Huduma za Habari ya mwaka 2016, nchini Tanzania ilikiuka vifungu 6(d) na 7(2) vya mkataba wa kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na uhuru wa kutoa maoni.

Hali kadhalika, EACJ iliitaka Tanzania kuhakikisha kuwa Sheria ya Huduma za Habari inarandana na mkataba huo.

EACJ ilianzishwa mwaka 2001 ikiwa na jukumu la kuhakikisha kuwa sheria zote ndani ya nchi wanachama zinatafsiriwa kulingana na mkataba wa kuanzishwa kwa jumuiya hiyo.

Pia hutoa maoni na ushauri wa kisheria, pamoja na kujihusisha kwenye usuluhishi.

TRT Afrika