Embu ni mojawapo ya kaunti ambapo madini ya Coltan yamepatikana nchini Kenya/ Picha Wizara wa Madini Kenya  

Kenya imetangaza kuwa madini ya coltan, ambayo hutumika kutengeneza vifaa vya umeme kama vile simu za mkononi, laptop na vifaa vingine vya mawasiliano yamepatikana nchini humo.

"Sasa ni rasmi. Tuna madini ya coltan nchini na tunataka kuona jinsi gani tunaweza kuhamasisha wawekezaji," Waziri wa Madini na Uchumi wa Bluu Salim Mvurya alisema Jumatano.

Madini hayo yamepatika katika kaunti sita nchini.

Waziri wa madini amesema hadi sasa matukio 970 ya madini yamebainika kote nchini, na uchimbaji utaanza hivi karibuni.

Serikali inapanga kuajiri wafanyakazi zaidi na kufungua maabara zaidi ili kusaidia katika uchunguzi wa madini hayo.

“Tutaweka huduma za maabara katika mikoa nane ambapo tutakuwa tunapima sampuli na kutangaza ubora wa madini yanayopatikana katika mkoa husika,” alisema.

Mchimba madini akionyesha madini ya coltan huko Birambo, eneo la Masisi, Mkoa wa Kivu Kaskazini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo/ Picha Reuters.

Bado haijulikani ni kiwango gani cha Coltan kipo nchini Kenya.

Madini ya Coltan ni yapi?

Haya ni madini ya chuma, ambayo mengi hupatikana mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Coltan hutumiwa zaidi katika utengenezaji wa bidhaa za kielektroniki zinazotumiwa kwa wingi, kama vile simu za rununu, kompyuta ndogo na vifaa vya michezo ya video, na ugunduzi huu utaipa hadhi Kenya kuwa moja wapo ya nchi zinazouza madini hayo nje ya nchi.

Wataalamu wanasema soko la kimataifa la coltan lilikuwa na thamani ya dola za Marekani milioni 1.5 mwaka 2019.

kufikia mwisho wa mwaka 2026, thamani ya soko la coltan linatarajiwa kufikia dola milioni 1.9, ambayo ni ukuaji wa kiwango cha asilimia 5.58 kwa mwaka kati ya 2021 na 2026.

Barani Afrika, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ina zaidi ya asilimia 70 ya madini aina ya Coltan duniani.

Katika soko ya kimataifa, bei ya coltan inategemea kiasi cha chuma cha tantalum kilichopo, lakini kwa wastani, kilo moja ya madini hayo inafikia zaidi ya dola 45.

TRT Afrika