Majeneza ya watoto 21 waliofariki katika ajali ya moto ya bweni katika Shule ya Hillside Endarasha Academy huko Nyeri / Picha: Reuters 

Ibada ya madhehebu mbalimbali ya kuwakumbuka wanafunzi 21 waliofariki kwenye ajali ya moto katika Shule ya Hillside Endarasha Academy huko Nyeri, imefanyika mapema hii leo huko nchini Kenya.

"Mioyo yetu ina uchungu sana kwa kufiwa na watoto 21 kwenye ajali ya moto ya Shule ya Hillside Endarasha," alisema Makamu wa Rais wa Kenya Rigathi Gachagua ambae alihudhuria ibada hiyo.

Maombi hayo yamefanyika katika uwanja wa Mweiga huko Kieni Magharibi, takriban Kilomita 24 kutoka Endarasha Hillside Academy ambapo mkasa huo ulitokea Septemba 6, 2024.

"Katika maombolezo makubwa na huzuni tunapata nguvu kidogo ya kusema jinsi tunavyohisi…tumevuka mito mingi hapo awali lakini huu ni mpana, wenye kina kirefu na wenye mafuriko," wawakilishi wa wanafunzi kutoka shule hiyo walisema katika ibada hiyo.

Lengo la ibada hiyo, lilikuwa ni kutoa heshima za mwisho kwa wanafunzi 21 walipoteza maisha yao kutokana na ajali hiyo.

Ndugu, jamaa na marafiki wa watoto wa waathirika walijumuika katika ibada hiyo maalumu. / picha : Reuters 

Taarifa kutoka shule hiyo, zinasema wakati wa ajali, bweni lilikuwa na wanafunzi wa kiume 156 .

Wiki iliyopita daktari wa uchunguzi wa serikali Johansen Oduor alithibitisha kwamba sampuli za vinasaba za waathiriwa zilichunguzwa na kulinganishwa na wazazi wao.

"Tumepokea matokeo ya wanafunzi 21 waliofariki katika ajali hiyo, na yamelingana na ya wazazi wao," alisema.

Bado chanzo cha moto hakijathibitishwa, huku uchunguzi ukiendelea.

Rigathi Gachagua Makamu wa Rais Kenya alihudhuria ibada hiyo / Picha:  Rigathi Gachagua

Ujumbe wa Rais wa zamani wa Kenya Uhuru kenyatta ulisomwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Mawaziri la Ulinzi Eugene Wamalwa.

"Kupoteza maisha ya vijana waliojaa uwezo na matumaini ya siku zijazo ni maumivu ambayo hayawezi kuelezewa. Moyo wangu unaenda kwa familia zilizopoteza watoto wao wapendwa na jamii ya shule iliyoathiriwa pakubwa na mkasa huu,” ujumbe wa Uhuru ulisema.

TRT Afrika