Bunge ya Kenya sasa imeunda kamati ya kufanya uchunguzi kuhusu kampuni hii ya kigeni / picha: Reuters

Mapema mwezi Agosti mwaka huu, maelfu ya Wakenya walijitokeza kwa ajili ya mboni zao za macho kukaguliwa na kampuni ya Worldcoin.

Waliokaguliwa walilipwa kwa sarafu za kidijitali.

Kampuni ya Worldcoin ilisema zaidi ya Wakenya 350,000 walijisajili.

Zoezi hili lilisimamishwa na serikali huku kukiwa na hofu kuwa data za wananchi zilikuwa zinakusanywa kwa madhumuni yasiyojulikana.

Bunge ya Kenya sasa imeunda kamati ya kufanya uchunguzi kuhusu kampuni hii ya kigeni.

Gabriel Tongoyo, Mwenyekiti wa Kamati hii ya bunge anasema wataalamu na mashahidi watafika mbele ya kamati ya wabunge wakati wa uchunguzi wake.

"Tunataka kuuliza juu ya uzingatiaji wa kisheria na udhibiti wa shughuli za Worldcoin na washirika wake, hatari ya kiafya inayoweza kusababishwa, matumizi yaliyokusudiwa ya data iliyokusanywa, na usalama wa ukusanyaji," Tongoyo amesema,

Wanaoongoza kwenye orodha ya mashahidi na wataalamu waliopangwa kufika mbele ya Kamati hiyo ni pamoja na gavana wa Benki Kuu ya Kenya, katibu wa baraza la mawaziri wa hazina ya kitaifa.

Watatarajiwa kuangazia uhusiano kati ya biashara ya sarafu wa kidijitali nchini Kenya na shughuli za hivi majuzi za Worldcoin miongoni mwa wengine.

Kamati hiyo ya wabunge saba pia inachunguza ikiwa Worldcoin ilitii sheria ya Kenya ya kulinda data, na sheria zingine husika nchini Kenya.

Wabunge hao pia watafanya mkutano na kampuni hiyo ya Worldcoin, ili kuelewa utendakazi wake na malengo ya mwisho ya zoezi lao la kukusanya data nchini Kenya.

TRT Afrika