Kenya imeanza utafiti kuhusu kuenea kwa ugonjwa wa matende/ Picha/ Wizara ya Afya Kenya           

Utafiti kuhusu ugonjwa wa matende au 'elephantisis' kwa kimombo unafanyika katika eneo la Lamu , Pwani ya nchi hiyo.

Matende ni ugonjwa wa kitropiki uliopuuzwa na maambukizi hutokea wakati vimelea aina ya minyoo vinapopitishwa kwa binadamu kupitia mbu.

Maambukizi ya kawaida hupatikana katika umri wa utotoni na husababisha uharibifu wa siri kwa mfumo wa lymphatic.

Ugonjwa huu huathiri miguu, mikono, figo, korodani na kusababisha korodani kuvimba na kuwa kubwa sana.

Mmoja wa wagonjwa wa matende.  Picha/ WHO

Mtu aliyeathirika miguu yake huvimba, pamoja na sehemu za siri.

Wataalamu wanaoongoza utafiti huo Pwani ya Kenya ni kutoka Wizara ya Afya ya Kenya, Shirika la Afya Duniani na Taasisi ya Utafiti wa Matibabu ya Kenya, KEMRI.

"Utafiti unalenga kukusanya takwimu muhimu kuhusu maambukizi ya matende miongoni mwa watu wazima ili kuendeleza safari ya mafanikio ya jumuiya kuelekea kutokomeza ugonjwa huo," Wizara ya Afya ya Kenya imesema.

Nchini Kenya, ugonjwa huu umeenea katika maeneo ya pwani ambayo ni pamoja na kaunti za Kilifi, Kwale, Mombasa, Taita Taveta na Tana River.

" Ugonjwa huu umetajwa kama ugonjwa wa kitropiki uliopuuzwa, tunatakiwa kufikia mahitaji ya WHO kuhakikisha kiwango cha maambukizi ya wadudu wanaoleta ugonjwa huu kinabaki chini ya asilimia 1 ndani ya jamii yetu," Wizara hiyo imeongezea.

Takriban watu milioni 120 duniani kote ambao ni asilimia 1.5 ya idadi ya watu duniani - wana maambukizi ya matende.

Kuna dawa za kusaidia waliathiriwa na matende.

Mtu anaweza kutumia dawa za kuzuia vimelea kama vile ivermectin (Stromectol), diethylcarbamazine (Hetrazan) au albendazole (Albenza).

Dawa hizi huharibu minyoo waliokomaa kwenye damu au kuizuia kuzaana.

Matumizi ya dawa pia yanaweza pia yanaweza kuzuia kupitisha maambukizi kwa mtu mwingine.

TRT Afrika