Serikali ya Kenya imetangaza kucheleweshwa kufunguliwa shule zote nchini humo kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, wizara ya elimu ilisema kuwa wamekusanya data na kuafikiana kuwa itakuwa kwa maslahi ya wanafunzi kuahirisha kufunguliwa shule.
''Athari mbaya za mvua katika baadhi ya shule ni kubwa sana hivi kwamba haitakuwa jambo la busara kuhatarisha maisha ya wanafunzi na wafanyikazi kabla ya hatua madhubuti za kuzuia maji kuchukuliwa ili kuhakikisha usalama wa kutosha wa jamii zote za shule zilizoathirika," alisema waziri wa elimu Ezekiel Machogu.
Wito wa wazazi
Tarehe mpya ya kufunguliwa shule sasa ni Mei 6, badala ya Jumatatu ya Aprili 29 kama ilivyokuwa katika ratiba ya awali.
Awali, chama cha wazazi nchini Kenya kilitoa wito kwa serikali kuzingatia kuahirisha kufunguliwa shule kutokana nahofu ya kiuhatarisha maisha ya watoto wao.
Haya yanajiri huku idara ya utabiri wa hali ya anga ikionya kuhusu mvua kubwa zaidi katika siku zijazo huku zaidi ya watu 90 wakiripotiwa kufariki na wengine wengi kujeruhiwa au kutoweka.
Mvua inayoendelea kunyesha imesababisha pia hasara kubwa ya miundo mbinu huku baadhi ya nyumba zikizamishwa kabisa, barabara kukatika na mito kufurika.
Baadhi ya shule hutumiwa kuwahifadhi wahanga waliokimbia makazi yao ambao nyumba zao zilisombwa na maji au kuharibiwa na mafuriko katika maeneo mengi ya nchi, hasa jijini Nairobi na maeneo mengine ya Kaskazini na Kaskazini Mashariki ambayo yameathirika zaidi.
Bado huenda tarehe hiyo mpya pia ikasogezwa mbele, kutokana na utabiri wa kuendelea kunyesha mvua kubwa nchini humo. Waziri wa elimu Machogu ameahidi kutoa taarifa zaidi kuhusiana na mabadiliko yoyote yatakayoibuka.